DCEA yapokea vifaa vya kisasa vya uchunguzi kutoka UNODC.
Na.Mwandishi wetu.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imepokea vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa kimaabara kutoka Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), ikiwa ni pongezi baada ya kutambua mafanikio yaliyofikiwa na Tanzania katika udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Akikabidhi vifaa hivyo tarehe 22 Aprili 2026 jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa UNODC Kanda ya Afrika Mashariki, Ali El-Bereir, aliipongeza Tanzania kwa jitihada zake katika kudhibiti biashara na matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kemikali bashirifu.
Vifaa hivyo vimetolewa mahsusi kuzijengea uwezo taasisi zinazoshughulikia udhibiti wa dawa za kulevya kimataifa kupitia mpango wa Port Security and Safety of Navigation Programme (EU PSP).
Miongoni mwa vifaa hivyo ni mashine za kisasa zenye uwezo wa kubaini kwa haraka aina mbalimbali za dawa za kulevya na kemikali zinazodhibitiwa, hata zikiwa ndani ya vifungashio vyake bila kufunguliwa, hatua itakayoongeza ufanisi wa uchunguzi na kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka.
Aidha, UNODC imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa kutoa mafunzo na kujenga uwezo kwa maafisa wa DCEA ili kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya dawa za kulevya.



Comments
Post a Comment