AFRIKA yaonywa kuhusu janga la magonjwa yasiyoambukiza.




Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam


Magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) yameendelea kuwa tishio kubwa kwa afya na uchumi wa nchi za Afrika, hali iliyochochea viongozi wa afya kutoa wito wa kuongeza uwekezaji katika kinga, matibabu na kuimarisha mifumo ya huduma za afya ili kuokoa maisha ya mamilioni ya wananchi.

Wito huo umetolewa leo juni 23,2026 katika Mkutano wa Tatu wa Kimataifa wa PEN-Plus Afrika 2026 unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa, alizitaka nchi za Afrika kuweka afya kuwa ajenda ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akifungua mkutano huo kwa niaba ya Rais Samia, Mchengerwa alisema magonjwa yasiyoambukiza kama kisukari, shinikizo la damu, saratani, magonjwa ya moyo, selimundu na changamoto za afya ya akili yamekuwa mzigo mkubwa kwa mataifa ya Afrika na yanahitaji hatua za pamoja za kuyadhibiti.

Alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa hayo husababisha zaidi ya vifo milioni 43 duniani kila mwaka, sawa na asilimia 74 ya vifo vyote, huku idadi kubwa ya vifo hivyo ikitokea katika nchi za kipato cha chini na cha kati.

Mchengerwa alisema Tanzania imeendelea kushuhudia ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, ambapo vifo vinavyotokana na magonjwa hayo vimeongezeka kutoka chini ya asilimia 25 katika miaka ya 1980 hadi kufikia asilimia 39 mwaka 2021.

Alibainisha kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na changamoto hiyo kupitia uwekezaji katika huduma za afya ya msingi, vifaa tiba na matumizi ya teknolojia ya kidijitali, huku asilimia 80 ya wananchi wakifikia huduma za afya ndani ya umbali wa kilomita tano kutoka makazi yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa WHO, Profesa Mohamed Janabi, alisema magonjwa yasiyoambukiza ni “janga linaloua kimya kimya” kwani hayapati uangalizi mkubwa kama magonjwa ya mlipuko licha ya kuendelea kusababisha vifo vingi kila siku.

Alisema kwa sasa takribani mtu mmoja kati ya wanne barani Afrika ana shinikizo la damu, mmoja kati ya 20 anaishi na kisukari na mmoja kati ya saba yupo katika hatari ya kupata saratani kabla ya kufikisha umri wa miaka 75.

Profesa Janabi aliongeza kuwa Afrika inapoteza karibu dola za Marekani trilioni moja kila mwaka kutokana na athari za magonjwa yasiyoambukiza kwa uzalishaji na gharama za matibabu, huku kiwango cha uwekezaji katika kukabiliana na magonjwa hayo kikiwa bado kidogo.

Alisisitiza kuwa mpango wa PEN-Plus umechangia kusogeza huduma za magonjwa sugu karibu na wananchi, ambapo zaidi ya watu 100,000 katika nchi zaidi ya 20 za Afrika tayari wananufaika na huduma hizo.

Naye Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Maghembe, alisema Tanzania inaendelea kuonyesha dhamira ya kuimarisha mifumo ya afya na kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa wa magonjwa yasiyoambukiza, jambo lililoifanya kuwa mwenyeji wa mkutano huo kwa mara ya pili.

Kwa upande wake, Ofisa Programu wa PEN-Plus kutoka taasisi ya Helmsley Charitable Trust, James Reid, alisema zaidi ya wagonjwa 170,000 barani Afrika wamenufaika na huduma za mpango huo, huku takribani nchi 20 zikiwa zimeanza au ziko katika hatua za kuutekeleza.

Washiriki wa mkutano huo wa siku tatu wanatarajiwa kujadili mikakati ya kuimarisha kinga, matibabu, upatikanaji wa dawa na teknolojia za afya, pamoja na kuongeza ushirikiano wa kikanda katika kupambana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza barani Afrika.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.