Bidhaa bandia zatajwa kutishia afya,uchumi na biashara halali

 



Na Mwandishi Wetu


Serikali imezitaka taasisi zote zinazohusika na udhibiti wa bidhaa nchini kuimarisha mapambano dhidi ya bidhaa bandia, hususan pombe, vilainishi na sigara bandia, ambazo zimeendelea kuhatarisha afya za wananchi, kuathiri biashara halali na kupunguza mapato ya Serikali.


Kauli hiyo imetolewa leo Juni 25,2026 na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kudhibiti Bidhaa Bandia Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam chini ya kaulimbiu isemayo “Linda maisha na masoko dhidi ya pombe, vilainishi na sigara bandia.”



Mapunda amesema biashara ya bidhaa bandia imekuwa changamoto kubwa inayohitaji ushirikiano wa wadau wote kutokana na athari zake kwa afya za wananchi, mazingira ya biashara na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Ameeleza kuwa licha ya juhudi zinazofanywa na Tume ya Ushindani (FCC), bado kuna haja ya kuongeza matumizi ya teknolojia za kisasa katika uchunguzi, ufuatiliaji na udhibiti wa bidhaa bandia, hasa katika masoko ya kidijitali na mipakani.

Aidha, ameagiza FCC kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano na taasisi nyingine za udhibiti, vyombo vya dola na mamlaka za forodha ili kubaini na kuziba mianya inayotumiwa na wahalifu wa kiuchumi kusambaza bidhaa bandia sokoni.

Kwa upande wake, Kamishna wa FCC, Said Tunda, amesema tume imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mpango mkakati wa miaka mitano uliomalizika, ikiwemo kuimarisha usimamizi wa ushindani, kulinda watumiaji na kudhibiti bidhaa bandia nchini.

Amesema kutokana na ongezeko la changamoto za bidhaa bandia, FCC imeandaa mpango mkakati mpya wa miaka mitano ambao umeweka eneo la udhibiti wa bidhaa bandia kuwa lengo mahsusi ili kuongeza ufanisi katika kugundua, kuzuia na kuondoa bidhaa hizo sokoni.

Tunda alibainisha kuwa maendeleo ya biashara mtandao, mabadiliko ya mifumo ya biashara na matumizi ya teknolojia mpya yameongeza changamoto katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia, hivyo kuhitaji uwekezaji mkubwa zaidi katika mifumo, teknolojia na rasilimali watu.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, amesema maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu madhara ya pombe, vilainishi na sigara bandia pamoja na kujenga ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi.

Alisema katika miezi ya hivi karibuni FCC imefanikiwa kukamata shehena mbalimbali za bidhaa bandia zikiwemo pombe, sigara na vilainishi ambazo zingesababisha madhara makubwa kwa watumiaji na uchumi wa nchi kama zingefika sokoni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani, Jaji Rose Ibrahim, alisema bidhaa bandia si tu kwamba zinapunguza mapato ya serikali bali pia zinadhoofisha uwekezaji halali na kuhatarisha maisha ya wananchi kutokana na viwango duni vya ubora.

Alihimiza wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa mbalimbali na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini bidhaa zenye viashiria vya kuwa bandia ili kusaidia juhudi za serikali katika kulinda afya za wananchi na kuhakikisha ushindani wa haki katika masoko ya Tanzania.

Maadhimisho hayo yaliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka taasisi za serikali, sekta binafsi, vyombo vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara pamoja na vyombo vya habari kwa lengo la kujadili mikakati ya pamoja ya kupambana na bidhaa bandia na kulinda masoko ya nchi.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.