NACTVET YATUMIA SABASABA KUTOA HAMASA YA ELIMU YA AMALI, YAWAONESHA WANAFUNZI WENYE UJUZI WA VITENDO
Na Mwandishi Wetu
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) linatumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake ya kusimamia ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, huku likitumia wanafunzi wa mkondo wa amali kuonesha matokeo ya maboresho ya mtaala wa elimu.
Akizungumza na waandishi wa habari juni 2,2026 Afisa habari NACTVET, Dora Tesha, alisema maonesho hayo yamekuwa fursa muhimu ya kuwafikia wananchi, wazazi na wadau mbalimbali kwa kuwapa elimu kuhusu huduma zinazotolewa na baraza pamoja na nafasi ya elimu ya amali katika kuwaandaa vijana kujitegemea.
Alisema jukumu kuu la NACTVET ni kusimamia utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kuhakikisha vyuo vinatoa mafunzo yenye viwango vinavyokubalika na yanayozalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.
Tesha alisema katika banda la NACTVET wananchi wanapata huduma mbalimbali ikiwemo taarifa kuhusu usajili wa vyuo, haki za wanafunzi, pamoja na elimu kuhusu mkondo wa amali ulioanzishwa kupitia maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la 2023.
Alieleza kuwa kuanzishwa kwa mkondo wa amali katika shule za sekondari kumewawezesha wanafunzi kupata ujuzi wa vitendo wakiwa bado shuleni, hatua inayowaandaa kujiajiri au kuendelea na masomo ya taaluma mbalimbali baada ya kuhitimu.
"Tumewaleta wanafunzi kwenye maonesho haya ili wazazi na wananchi wajionee wenyewe uwezo wao. Wapo wanaofanya kazi za umeme, kuchora ramani za majengo na kutengeneza miradi mbalimbali. Haya ni matokeo ya uwekezaji uliofanywa kwenye elimu ya amali," alisema Tesha.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu kutoka Shule ya Sekondari Baobab anayesoma mkondo wa amali katika fani ya umeme alisema mfumo huo umemjengea uwezo wa vitendo na kumpa matumaini ya kutimiza ndoto zake za kuwa mhandisi siku zijazo.
Alisema mafunzo hayo yamewapa wanafunzi nafasi ya kuandaa miradi mbalimbali ya umeme na kuwahimiza Serikali kuendelea kuupanua mkondo wa amali katika shule nyingi zaidi.
Kwa upande wake, mwalimu wa taaluma ya amali katika Shule ya Sekondari Baobab, Philip Razalo, alisema mkondo huo unawajengea wanafunzi uwezo wa kujiajiri na kuanzisha biashara zao badala ya kusubiri ajira rasmi baada ya kuhitimu masomo.
Naye mwanafunzi wa mafunzo ya amali kutoka shule sekondari ya bwiru Daud Elias, alisema elimu hiyo imemwezesha kujifunza kuchora ramani za majengo na kuelewa hatua mbalimbali za ujenzi, akisisitiza kuwa kuimarishwa kwa mkondo wa amali kutazalisha vijana wengi wenye ujuzi watakaochangia maendeleo ya uchumi wa taifa.




Comments
Post a Comment