Serikali yatumia Sabasaba kusogeza huduma, kutatua kero za wananchi.
Na.Mwandishi wetu.
WANANCHI wametakiwa kutumia Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu ili kupata huduma mbalimbali za Serikali, kuwasilisha kero zao na kupatiwa ufumbuzi pamoja na elimu kuhusu fursa za maendeleo.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, alipotembelea banda la Ofisi hiyo katika maonesho hayo, akisema Serikali imejipanga kuhakikisha huduma muhimu zinawafikia wananchi kwa urahisi na kwa wakati.
Alisema banda hilo limekusanya taasisi mbalimbali chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), hatua inayowezesha wananchi kupata huduma nyingi katika eneo moja bila usumbufu.
"Tunawakaribisha wananchi wote kufika katika banda letu kupata elimu, huduma mbalimbali za Serikali na kuwasilisha changamoto zao ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati," alisema Profesa Kabudi.
Alieleza kuwa wataalamu waliopo bandarini wanatoa ushauri kuhusu elimu, ajira, hifadhi ya jamii, uwekezaji, biashara na huduma nyingine, huku baadhi ya changamoto zikitatuliwa papo hapo na nyingine kupewa mwongozo wa namna ya kuzifikisha kwenye mamlaka husika.
Profesa Kabudi alisema vijana waliomaliza kidato cha nne wanapatiwa ushauri kuhusu uchaguzi wa tahasusi kabla ya kujiunga na kidato cha tano, wakati taasisi za hifadhi ya jamii zikiendelea kutoa elimu kuhusu usajili, mafao na huduma nyingine kwa wananchi.
Aliongeza kuwa maonesho ya mwaka huu yanafanyika sambamba na kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo wananchi wanapata nafasi ya kujionea mafanikio ya Serikali na kufahamu fursa mbalimbali zitakazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Comments
Post a Comment