TOSCI yafungua milango ya soko la kimataifa kupitia mbegu bora

 



Na.Mwandishi wetu


Taasisi ya Udhibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imesema Tanzania imejijengea uwezo wa kuzalisha mbegu bora zinazokubalika katika masoko ya kimataifa, hatua inayofungua fursa mpya kwa wakulima na wawekezaji kunufaika na biashara ya mbegu ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, alisema mafanikio hayo yametokana na uwepo wa maabara ya taifa yenye ithibati ya kimataifa inayohakikisha mbegu zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vinavyotambulika duniani.

Alisema uwezo huo unaenda sambamba na ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha kilimo biashara kupitia matumizi ya mbegu bora, ambazo ni msingi wa kuongeza uzalishaji na ushindani wa mazao katika soko la kimataifa.

Chimagu alisema jukumu la TOSCI ni kusajili aina mpya za mbegu, wazalishaji pamoja na mashamba ya uzalishaji huku ikifanya ukaguzi katika kila hatua ili kuhakikisha mbegu zinazowafikia wakulima zina ubora unaotakiwa.

Alieleza kuwa taasisi hiyo pia imeanzisha mfumo wa kidijitali unaomwezesha mkulima kuhakiki uhalali wa mbegu kwa kutumia simu ya mkononi kupitia namba 14852#, kwa kuingiza namba iliyopo kwenye lebo ya TOSCI.

Aidha, alisisitiza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mbegu, ni marufuku kuuza mbegu ambazo hazijafungashwa au zisizo na lebo ya uthibitisho wa TOSCI, akiwataka wananchi kutoa taarifa wanapobaini mbegu zenye shaka ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Alisema matumizi ya mbegu bora huchangia kuongeza mavuno, kuboresha ubora wa mazao na kuwawezesha wakulima kuzalisha kwa tija zaidi, jambo linalokuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Kupitia ushiriki wake katika maonesho ya Sabasaba, TOSCI inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uzalishaji, uthibitishaji na biashara ya mbegu bora pamoja na fursa zilizopo katika masoko ya ndani na ya kimataifa.



Chimagu aliwahimiza wakulima, wawekezaji na wadau wa sekta ya kilimo kutembelea banda la TOSCI ili kujifunza kuhusu teknolojia za mbegu bora na kutumia fursa zilizopo kukuza kilimo biashara chenye ushindani wa kimataifa.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.