BoT YANG'AA TUZO YA UBUNIFU KATIKA HUDUMA JUMUISHI ZA KIFEDHA.
Na Sophia Kingimali
Benki kuu ya Tanzania( BoT)imetunukiwa Tuzo kuu ya ubunifu katika huduma jumuishi za kifedha ambapo tuzo hiyo imetokana na ubunifu wa mifumo ya malipo ikiwemo mfumo wa TIPS(Tanzania Instant Payment System) na TANQR(QR Code ya kitaifa ya malipo).
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 16,2025 jijini Dar es Salaam wakati akitangaza tuzo hiyo Mkurugenzi wa Mifumo ya malipo ya Taifa Lucy Shaidi amesema tuzo hiyo imetolewa na Jumuiya ya huduma Jumuishi za Fedha(AFI) yenye wanachama 84 duniani imetokana na juhudi za BOT katika ubunifu uliofanywa wa kiteknolojia katika kufanikisha uchumi wa kidigital.
"Mfumo huu wa TIPS umesaidia kupunguza gharama za miamala kwa wananchi huku mfumo wa TANQR ukiwarahisishia wafanyabiashara kupokea malipo kupitia benki na makampuni ya simu hivyo mfumo huu umewavutia mataifa mengi ya jirani",Amesema.
Ameongeza kuwa tayari BoT imeshatoa ujuzi huo kwa nchi ya Kenya,Lesotho,Rwanda na Uganda huku burundi ikiwa inatarajiwa kupata mafuzo hayo hivi karibuni.
"Kwa mujibu wa Takwimu mfumo wa TIPS umewezesha ongezeko la miamala kufikia milioni 560 yenye thamani ya shilingi Trilioni 41 kwa mwaka wa fedha 2024-2025 sambamba na kuanzisha mazingira ya majaribio ya ubunifu yanayowezesha wabunifu wa teknolojia kujaribu bunifu zao kabla ya kuzifikisha sokoni",Amesema.
Sambamba na hayo amesema wamezindua mfumo unaofahamika kwa jina la SEMA na BoT wenye lengo la kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za kifedha nchini.
Kwa upande wake Meneja msaidizi wa kurugenzi ya mifumo ya malipo ya Taifa Mutashobya Mushumbusi amesema tuzo hiyo ni ya heshima kubwa kwa nchi hivyo inatoa motisha kwa watendaji kuendelea kutumia ubunifu na teknolojia ili kufanikisha uchumi wa kidigital.
Pia ameongeza kuwa mpaka sasa asilimia 76 ya watanzania kwa sasa wanapata huduma ya jumuishi za kifedha kwani lengo likiwa kufikia mwaka 2028 asilimia 85 wawe wanatumia huduma hizo.
Tuzo hiyo ilitolewa katika mkutano mkuu wa AFI uliofanyika hivi karibuni mjini Swakopmund nchini Namibia na ilipokelewa na Naibu gavana wa BoT anayeshughulikia uthabiti na usimamizi wa Sekta wa sekta ya Fedha Sauda Msemo kwa niaba ya Gavana Emmanuel Tutuba.







Comments
Post a Comment