DIWANI KATA YA NDUGUMBI AHAIDI MAKUBWA AWATAKA WANANCHI KUMUAMINI NA KUMCHAGUA.
Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kata ya Ndugumbi wamewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ifikapo tarehe 29 ili kukamilisha ushindi wa chama hicho katika ngazi zote za uongozi.
Wito huo umetolewa jijini Dar es salaam wakati wa uzinduzi wa kampeni za udiwani katika kata hiyo mkutano uliohudhuriwa na wanachama na wafuasi wa CCM, ambapo mgombea wa udiwani wa kata hiyo, Amina Mtevu, alitambulishwa rasmi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, Abasi Mtevu, amewakumbusha wananchi kuwa siasa ni maisha na ni lazima viongozi wasikilize na kutatua changamoto za wananchi.
Pia amewataka wananchi kutokuridhika tu kwa imani kuwa CCM itashinda, bali wajitokeze kupiga kura ili chama kipate ushindi wa heshima.
“Msiache kwenda kupiga kura. Ushindi wa heshima unahitaji kila mmoja kujitokeza octoba 29 mapema kwenda kupiga kura kwa kuchagua viongozi wa CCM,”amesema.
Kwa upande wake Mgombea wa udiwani, kata ya Ndugumbi Amina Mtevu, amewaomba wananchi wamwamini na kumpa nafasi ya kuendeleza maendeleo katika kata ya Ndugumbi.
Aidha ameahidi kuendelea kusimamia upatikanaji wa mikopo kwa wanawake na vijana, kushughulikia changamoto za mto Mwangosi unaosababisha mafuriko, na kuhakikisha miradi ya barabara za ndani inakamilika kwa wakati.
“Uongozi haujaribiwi,” amesema Amina, “Nawaomba mniamini, nami nitahakikisha maendeleo yanafika kila kona ya Ndugumbi.”
Awali Mwenyekiti wa vijana wa CCM(UVCCM)mkoa wa Dar es Salaam Nasra Mohammed ameongeza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameendeleza na kukamilisha miradi yote iliyoanzishwa na watangulizi wake, ikiwemo kushughulikia tatizo la maji kupitia mradi wa bwawa la Kidunda, ambao sasa umefikia asilimia 3 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2026.
Alitaja pia kwamba serikali imeanza kuboresha miundombinu ya mkoa huo kupitia barabara za mwendokasi na mipango ya ujenzi wa reli za ndani kutokana na ongezeko la watu na magari.
Vilevile, amebainisha kuwa zaidi ya bilioni 60 zimetengwa kama mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, huku milioni 300 zikitengwa kuboresha masoko na kujenga soko jipya Ndugumbi. Hata hivyo, sehemu ya fedha hizo ilielekezwa upya kutengeneza soko la Kawe lililoungua moto.
Katibu wa CCM kata ya Ndugumbi, Christina Gama amesema kuwa CCM imekuwa ikishinda mara zote katika kata hiyo na safari hii wanaamini ushindi huo utadumishwa.
Amefafanua kuwa awali kulikuwa na wagombea saba waliowania nafasi ya udiwani, lakini baada ya mchujo na kikao cha maridhiano, Amina Mtevu alipatikana kuwa mgombea wa chama.
“Makundi yote sasa yamevunjwa, tumeungana kuhakikisha kura zote zinakwenda kwa wagombea wetu na chama,” amesema.
Awali aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Masawe, aliwaeleza wananchi kuwa CCM imefanikisha maendeleo makubwa katika kata hiyo ambapo ametaja mafanikio makuu matatu ambayo ni ujenzi wa Kituo cha Afya, maboresho makubwa katika shule tatu za kata hiyo, na ujenzi wa barabara nyingi kwa kiwango cha lami na zege.
Ameongeza kuwa madarasa 12 na vyoo vipya vimejengwa, na wanafunzi sasa wanapata huduma ya chakula shuleni, yote ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya CCM.
Viongozi wa CCM wamesisitiza mshikamano na amani wakati wa uchaguzi huku wakiwataka wananchi kuhakikisha wanakamilisha “mafiga matatu” kwa kupiga kura za Urais, Ubunge, na Udiwani ili maendeleo yaliyoanza kuonekana yaendelee.










Comments
Post a Comment