MGOMBEA URAIS WA NLD DOYO HASSAN APOKEWA KWA DUA NA WAZEE WA MISIMA, WILAYA YA HANDENI
Handeni, Tanga
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amepokelewa kwa heshima ya kipekee na kufanyiwa dua maalum na wazee wa Kijiji cha Misima, Wilaya ya Handeni, mkoani Tanga.
Wazee wa kijiji hicho walijitokeza kwa wingi kumpokea Doyo na kumfanyia dua za kumtakia kheri, baraka, na mafanikio katika safari yake ya kisiasa ya kuwania nafasi ya juu kabisa ya uongozi wa taifa.
Akizungumza kwa niaba ya wazee wa Misima, mmoja wa viongozi wa kidini alisema, “Misima ni sehemu yenye historia kubwa ya mapambano ya ukombozi wa taifa hili. Tunamwona Mhe. Doyo kama kijana aliyepita katika nyayo zile zile za wazee wake waliopigania uhuru. Uthubutu wake ni wa kipekee na utakumbukwa na vizazi vijavyo hapa Misima.”
Kwa upande wake,Doyo aliwashukuru wazee hao kwa mapokezi yao yenye heshima na maombi yao ya baraka, akiwataka waendelee kumuombea usiku na mchana ili dhamira yake ya kulitumikia taifa iweze kutimia kwa neema ya Mwenyezi Mungu. “Naomba mzidi kuniombea. Dua zenu ni silaha yangu. Nipo kwenye dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania, na ninaamini kuwa kwa msaada wa Mungu na wazee wangu, jambo hili litatimia,” alisema Mhe. Doyo kwa unyenyekevu.
Ziara hiyo ni sehemu ya mfululizo wa safari ya kuelekea katika uzinduzi rasmi wa kampeni za kitaifa za chama cha NLD, zinazotarajiwa kufanyika mkoani Tanga mnamo tarehe 4 Septemba 2025.
Mhe. Doyo akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa chama hicho, wanaeelekea jijin Tanga tayari kwa maandalizi ya tukio hilo kubwa la kisiasa la uzinduzi wa kampeni ambazo zitaleta matumaini mapya kwa wananchi wengi wa Tanga na Tanzania kwa ujumla.



Comments
Post a Comment