KINYOGOLI AWATAKA WANANCHI MBAGALA KUCHAGUA MAENDELEO.

 


Na Sophia Kingimali.


MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Mbagala kupitia Chama cha Wananchi (CUF),Sheik Said Kinyogoli, ameahidi kupigania maslahi ya wananchi wa jimbo hilo endapo atachaguliwa kuwa Mbunge katika uchaguzi mkuu ujao, akisisitiza kuwa muda wa maneno umeisha na sasa ni wakati wa matendo.


Akizungumza wakati wa kufunga kampeni zake za ubunge katika jimbon hilo zilizofanyika jana katika eneo la Mbagala Kijichi, Kinyogoli amesema wananchi wa jimbo hilo wanahitaji kiongozi atakayesimama kuwasemea bungeni na sio wabunge wanaokaa kimya bila kuchangia hoja muhimu.


“Jimbo letu lazima lipate mtu wa kulipigia kelele ili tupone. Tunaambiwa elimu bure, lakini wazazi bado wanachangia hadi mishahara ya walimu. Mwaka huu hatucheki na yeyote, tunataka ushindi ili tuiseme Mbagala yetu,” alisema Kinyogoli huku akishangiliwa na umati wa wananchi.

Aidha, Kinyogoli amewataka wananchi kuachana na ushabiki wa vyama na badala yake kumchagua kiongozi mwenye uwezo wa kuwatumikia kwa vitendo.


“Sasa hivi hatuhitaji ushabiki wa vyama, tunahitaji mtu atakayetusaidia na kutusemea. Kamchagueni Kinyogoli ili Mbagala iwe jimbo la mfano ambapo wengine watakuja kujifunza,” ameongeza.


Katika mkutano huo, Kinyogoli pia amewaahidi waendesha bodaboda  kuwa ndani ya miezi mitano baada ya kuchaguliwa, hakuna atakayekamatwa kwa kukosa leseni, kwani atahakikisha kila dereva anapata leseni huku akiahidi ujenzi kituo maalumu cha kuwajengea uwezo vijana na  kubadilisha fikra zao.

Kwa upande wake, Katibu wa CUF Jimbo Mbagala Ibrahim Bakonzi, amesema chama hicho kimeendesha kampeni zake kwa amani tangu Tume ya Uchaguzi ilipotangaza ratiba, na kwamba wamepata mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wa Mbagala.


“Tumefanya kampeni vizuri kwa njia zote, na wote wanamuunga mkono Said Kinyogoli. Hata baadhi ya viongozi wa CCM wameonyesha wazi kutambua uwezo wake. Kazi imeisha, tunasubiri ushindi,” amesema Bakonzi.


Bakonzi alimshukuru mgombea kwa kujitolea muda na rasilimali zake katika kuhakikisha anasimamia maslahi ya wananchi, akimkumbusha kuwa ana deni kubwa kwa wananchi kutokana na upendo waliomwonyesha tangu mwanzo wa kampeni.

Wakati huo huo, Mgombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni, Wakili Msomi Mohamed Majaliwa, amewataka wananchi wa Kigamboni kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani, akisema kuwa hakuna sababu ya vurugu au maandamano.


“Kazi tumeshaimaliza. Jitokezeni mpige kura, hakuna vurugu. Wabunge hatutaki kuongoza walemavu wa kujitakia; kazi yetu ni moja tu, kupiga kura na kusubiri matokeo,” amesema Majaliwa.


Akihitimisha, Bakonzi ameliomba Jeshi la Polisi kuhakikisha ulinzi wa watu na mali katika vituo vya kupigia kura, na kusisitiza kuwa haki itawale wakati wa kutangaza matokeo.

“Tunawaomba polisi wasimamie haki itendeke. Mgombea atakayeshindwa atangazwe kwa haki. Mkikataa, tutalazimika kudai haki hiyo,” amesema.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.