SERIKALI YAWATAKA WATANZANIA KUDUMISHA AMANI NCHINI.



Na Sophia Kingimali.


Serikali imewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, ikisisitiza kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba huku kulinda amani ni wajibu wa kila Mtanzania.


Akizungumza kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, ,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo, alitoa wito huo katika Kongamano la Kitaifa la Amani lililofanyika Leo Octoba 27,2025 jijini Dar es Salaam, likiwa na kaulimbiu “Kupiga kura ni haki yetu, kuilinda amani ni wajibu wetu.”


Prof. Mkumbo amewahimiza Watanzania kutumia uchaguzi kama jukwaa la kuimarisha maendeleo na utulivu wa taifa. 


“Maendeleo ni mchakato endelevu. Tutumie uchaguzi huu kuwachagua viongozi watakaotupeleka mbele katika dira ya amani na maendeleo tunayoitamani,” amesema.


Prof. Mkumbo ameishukuru Kamati ya Amani ya Kitaifa kwa kuandaa makongamano hayo nchini kote, kwani  yamerudisha imani kubwa miongoni mwa wananchi kwa taasisi za dini na viongozi wa serikali. “Watanzania wengi wanaamini sana viongozi wa dini, kisha Rais, halafu Jeshi. Hivyo, mmefanya jambo kubwa kwa kusaidia nchi yetu katika kipindi hiki nyeti,” amesema.



Ameongeza kuwa serikali inatambua mchango wa viongozi wa dini katika kuhimiza maombi na mazungumzo ya amani, akibainisha kuwa mafanikio mengi yaliyopatikana nchini ni matokeo ya maombi ya Watanzania. “Kwa niaba ya serikali, nawapongeza na kuwashukuru kwa kuendelea kuiombea nchi yetu, viongozi wetu na Watanzania kwa ujumla,” alisema Prof. Mkumbo.


Akizungumzia uchaguzi ujao, amesema Tanzania ipo katika maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 14 tangu uhuru, na kwamba hakuna uchaguzi wowote uliowahi kukosa changamoto, lakini daima nchi imeendelea kudumisha amani na utulivu. “Huu ni uchaguzi wa saba tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi, na yote yamekuwa yakifanyika kwa amani. Tunapaswa kumwomba Mungu uchaguzi huu nao uwe wa amani,” amesisitiza.


Prof. Mkumbo alisema uchaguzi ni fursa muhimu ya kutafakari historia na mustakabali wa taifa, akiwahimiza Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura. “Uchaguzi unahusisha tunu zetu za taifa: utu, haki, usawa, upendo, umoja, demokrasia, muungano na amani. Hizi ndizo nguzo zinazoitambulisha Tanzania,” amesema.

Sambamba na hayo ameonya kuwa Watanzania wasizoe amani wakidhani ni jambo la kawaida, kwani ikipotea, ni vigumu kuirejesha. “Amani ni msingi wa kila jambo. Maendeleo, demokrasia na hata ibada haviwezi kudumu bila amani,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mohamed Makusi, amesema Jeshi la Polisi litaendelea kufanya kazi kwa weledi mkubwa kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya amani na usalama. “Tutahakikisha kila mwenye haki ya kupiga kura anapiga kwa utulivu, na nchi yetu inabaki salama hata baada ya uchaguzi,” alisema Makusi.


Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano, Sheikh Alhad Mussa, amewaomba viongozi wa dini na wazazi kuendelea kuwaelimisha vijana kuhusu thamani ya amani. “Vijana wafahamu hawana nchi nyingine zaidi ya Tanzania. Kuiharibu amani ni rahisi, lakini kuirejesha ni vigumu. Tuwasihi wasikubali kupotoshwa,” amesema Sheikh Mussa.


Kwa upande wake, Rais wa Taasisi ya Amani,maridhiano na maendeleo Ya AFREDA Dkt.Denis  Muchunguzi, amesisitiza kuwa taifa la Tanzania ni moja na linapaswa kulindwa kwa nguvu zote. “Tukiliacha likizama, tutazama sote. Amani ni takwa la maisha, katiba na dini zetu,” amesema.


Kongamano hilo limewaleta pamoja viongozi wa dini, serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, na wawakilishi wa asasi za kiraia, likiwa ni sehemu ya maandalizi ya kitaifa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.