Viongozi wa Serikali katika mitaa na kata ni chachu ya maendeleo:DC Mpogolo.
Na Sophia Kingimali
Mkuu wa wilaya wa Ilala Edward Mpogolo amesema serikali inatambua na kuthamini
Ushirikiano unaoendelea kati ya viongozi wa serikali za mitaa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), katika kuhakikisha huduma za umeme zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa ufanisi.
Hayo ameyasema leo Novemba 20,2025 wakati akifungua mafunzo maalumu kwa viongozi wa kata na mitaa,
Amesema viongozi wa serikali za mitaa wana nafasi ya kipekee katika kusimamia masuala ya umeme kwa kuwa wao ndio wapo karibu na wananchi hivyo viongozi wanapaswa kuwasaidia wananchi kufahamu hatua sahihi za kutoa taarifa za hitilafu za umeme kupitia mfumo mpya wa Nihudumie, ambao unatoa huduma kwa haraka na bila gharama.
"Viongozi ni watu muhimu katika kusimamia ulinzi wa miundombinu ya umeme, ikiwemo nguzo na nyaya, hasa katika maeneo ya mijini ambayo yanakabiliwa na uharibifu kutokana na shughuli za ujenzi ambapo baadhi ya uharibifu huo husababishwa na watu wanaounganisha umeme kiholela, kitendo kinacholeta madhara kwa jamii na kuilazimu TANESCO kubeba lawama zisizostahili"Amesema.
Akizungumzia Wajibu wa viongozi wa mitaa, amesema suala la umeme ni miongoni mwa changamoto kubwa za wananchi, hivyo viongozi wanapaswa kushirikiana kikamilifu kuhakikisha matatizo hayo yanatatuliwa kwa kushirikiana na TANESCO.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja, Irene Gowele, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO LazaroTwange, amesema TANESCO imeanzisha mkakati wa kushirikiana kwa karibu na viongozi wa mitaa ili kuboresha upatikanaji wa taarifa, kuharakisha huduma na kutatua changamoto za umeme kwa ufanisi zaidi hivyo kupitia mafunzo na majadiliano yao ya leo, viongozi hao wataelezwa miradi ya kimkakati inayoendelea katika maeneo yao na namna wanavyoweza kuwa daraja la mawasiliano kati ya wananchi na shirika.
“Viongozi hawa ndio macho na masikio ya serikali katika maeneo yao. Tukifanya kazi nao kwa karibu, tunawafikia wananchi haraka na kwa uhakika zaidi,” amesema Gowele.
Naye, Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Dar es Salaam, Juma Abbas Mwegamno, ameishukuru TANESCO kwa kushirikisha viongozi hao na kuwapa elimu kuhusu utekelezaji wa miradi ya umeme ambapo hatua hiyo imewapa uwezo wa kurudisha taarifa sahihi kwa wananchi, kama inavyoelekezwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu wajibu wa mamlaka za umma.
Mwegamno ameongeza kuwa hatua ya TANESCO kuonyesha maendeleo ya miradi mikubwa, ikiwemo Bwawa la Julius Nyerere ambalo limekamilika kwa asilimia 100 na kuzalisha megawati 115,000, imetoa matumaini makubwa katika upatikanaji wa nishati ya uhakika nchini.
Amesema jitihada hizo zinaendana na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutumia nishati safi na bora kwa maendeleo ya kaya na viwanda.







Comments
Post a Comment