WAZIRI AIPONGEZA BRELA KWA KUBORESHA MIFUMO NA KUONGEZA UFANISI.

 


Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga, ameipongeza Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) kwa hatua kubwa za kuboresha mifumo ya utoaji huduma ili kuendana na dira ya Serikali katika masuala ya Biashara na Uwekezaji.


Akizungumza katika ziara yake aliyoifanya kwenye ofisi za BRELA, leo tarehe 27 Novemba 2025 Mhe. Kapinga alisema Serikali inaendelea kushuhudia mapinduzi makubwa ya kiteknolojia kwenye sekta ya viwanda, hivyo ni muhimu taasisi zinazohusiana moja kwa moja na biashara kuendelea kuboresha huduma zake.


"Tuko kwenye mapinduzi makubwa ya kiteknolojia, katika kipindi kama hiki huwezi kuacha kuzungumzia teknolojia inayorahisisha mazingira ya kufanya biashara. Nawapongeza kwa maboresho makubwa ya mifumo ambayo imeleta tija kwa kiasi kikubwa," alisema Waziri Mhe. Kapinga


Aidha, alieleza kuwa mpango wa maendeleo wa nchi unakusudia kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa trilioni dola na kwamba hilo linawezekana kwa kuweka mazingira rafiki ya kufanya biashara, kupunguza gharama na muda wa kuanzisha na kuendesha biashara, pamoja na kuwa na taasisi za umma zenye ufanisi na mifumo ya kidijitali inayounganishwa kikamilifu.


"Ninaamini BRELA ni lango kuu la kuingia kwenye uchumi wa soko, ndiyo mlango wa kwanza wa usajili wa makampuni, majina ya biashara, na mlinzi wa haki za miliki bunifu, alama za biashara na miundo bunifu ya viwandani," alieleza Mhe. Kapinga 


Katika miaka hii mitano, matarajio ya Rais ni makubwa sana, ameahidi ajira milioni nane, mitaa ya viwanda kila wilaya na fedha za mfuko wa vijana kwa ajili ya kuchochea ajira, hatua zote hizi chanzo chake ni hapa BRELA. 


Vile vile Waziri Kapinga aliongeza kuwa mafanikio ya uwekezaji yamejikita katika namna taasisi kama BRELA zinavyorahisisha taratibu za biashara na kusisitiza kuwa dira ya mwaka 2050 inalenga mafanikio ambayo Serikali inaamini yanaweza kufikiwa kwa kuwekeza kwenye ubunifu, sekta binafsi na teknolojia. 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amemshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Salvio Kapinga kwa kutembelea Wakala na kujionea jinsi majukumu yanavyotekelezwa akisema ujio wake umeleta hamasa kubwa kwa watumishi na uongozi katika kuendelea kuboresha huduma kwa wananchi.


Bw. Nyaisa ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote pamoja na ushauri uliotolewa, ili kuongeza ufanisi na kuimarisha utendaji kazi wa taasisi, hususan katika maeneo ya mifumo ya kidijitali na utoaji wa huduma kwa wakati.


“BRELA katika utekelezaji wa majukumu yetu, asilimia karibu 90 tunategemea mifumo. Mifumo yetu imeunganishwa na taasisi nyingi za msingi kama vile NIDA, TRA na Mabenki. Mifumo yetu inasomana; kwa mfano, huwezi kwenda kukopa benki bila wao kuomba taarifa zako BRELA,” alisema Bw. Nyaisa.


Ameeleza kuwa uhusiano huu wa kimfumo unalenga kurahisisha huduma, kuongeza uwazi, kupunguza mianya ya udanganyifu, na kuhakikisha taarifa zinazotolewa kwa wadau mbalimbali zinakuwa sahihi na zinapatikana kwa wakati.



Aidha, Bw. Nyaisa alisisitiza kuwa BRELA itaendelea kuboresha mifumo yake ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na mahitaji ya sekta ya biashara nchini, sambamba na kuunga mkono malengo ya Serikali ya kujenga uchumi shindani na jumuishi kuelekea mwaka 2050.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.