MIAKA MINNE YA UONGOZI WA RAIS DKT.SAMIA MIRADI YA UWEKEZAJI IMEONGEZEKA;PROF.KITILA

 


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam


KATIKA kipindi cha miaka minne(2021-2025) ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa imeongezeka kutoka 252 kwa mwaka hadi kufikia miradi 901 kwa mwaka.

Aidha, kiwango cha mitaji ilivyovutiwa kuingia nchini iliongezeka kutoka Dola za Kimarekani Bilioni 3.7 mwaka 2021 hadi kufikia Dola bilioni 9.3 mwaka 2024.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, uliolenga kutoa mwelekeo wa kisera na kiutendaji wa Serikali kupitia Wizara ya Mipango na Uwekezaji kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, serikali imeweka vigezo vitatu katika uwekezaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo ambayo ni idadi ya miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa, idadi ya ajira zilizozalishwa kupitia miradi iliyosajiliwa pamoja na mtaji uliovutiwa kutokana na miradi hiyo.

Alisema katika kuhamasisha, kuvutia, kuwezesha na kuimarisha uwekezaji nchini, Serikali itandelea kuimarisha Kituo cha Mahala Pamoja (One Stop Facilitation Centre).

“Kituo hiki kwa sasa kina jumla ya taasisi 14 za umma zinazotoa huduma katika jengo moja kwa lengo la kuondoa urasimu, kupunguza muda, gharama na usumbufu kwa wawekezaji kuzunguka ofisi moja hadi nyingine,”alisema.

Pia kuimarisha na kukuza Benki ya Ardhi ambapo kwa mujibu wa Sheria Na. 6 ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi ya Mwaka 2025, Mamlaka ya Uwekezaji na maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania(TISEZA) imepewa jukumu la kuanzisha benki ya ardhi kwa kushirikiana na wizara yenye dhamana ya ardhi pamoja na mamlaka za serikali za mitaa.

“Hadi sasa (2025), TISEZA inamiliki ardhi yenye ukubwa wa Hekta 170,176.96 kwa ajili ya uwekezaji, ikijumuisha mashamba na maeneo maalum ya kiuchumi,”alisema.

Alisema hadi sasa kuna mashamba matano yanayomilikiwa na TISEZA yana ukubwa zaidi ya ekari 78,144.35, Viwanja na Mashamba yaliyowasilishwa kutoka kwenye Taasisi za Serikali na halmashauri ni zaidi ya 202 na viwanja vilivyowasilishwa na sekta binafsi 124.

Prof Kitila alisema miaka mitano ijayo, Serikali itaanzisha Jukwaa la Uwekezaji la Kitaifa (National Investment Forum) kwa ajili ya kukutana na wawekezaji wote na kufanya tathmini ya maendeleo ya uwekezaji nchini.

“Kuanzia Januari 2026, TISEZA itakuwa na jukumu la kuratibu jukwaa hili ambalo litahusisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Waziri wa Viwanda na Biashara, Waziri wa Fedha, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Waziri wa Muungano na Mazingira na taasisi husika za umma ili kukutana na wawekezaji kwa dhumuni la kufanya tathmini ya maendeleo ya uwekezaji nchini, kusikiliza changamoto, kupokea maoni, na kuyafanyia kazi,”alisema.

Kiongozi huyo alisema kwa kuzingatia malengo na matarajio ya Dira 2050, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, miradi ya uwekezaji itachaguliwa kwa kuzingatia vigezo ambavyo ni uwezo na fursa ya kuzalisha ajira kwa wingi, uwezo na fursa ya kuongeza mauzo ya nje.

Aliongeza nafasi ya sekta kukua na kuchochea ukuaji wa sekta nyingine, nafasi ya sekta katika kuongeza thamani, fursa ya sekta katika kukuza mapato ya serikali.

Aidha kwa kuzingatia vigezo hivyo, kipaumbele katika uwekezaji kitatolewa katika maeneo 10 ambayo ni kilimo na uchakataji wa mazao ya kilimo, uzalishaji wa bidhaa muhimu kwa matumizi ya ndani na ambazo tunaagiza zaidi kutoka nje.

“Bidhaa hizi ni pamoja na uzalishaji wa dawa na vifaa tiba, mafuta ya kupikia na ngano. Tutakaribisha, kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji katika kujenga kiwanda cha kukamua mafuta ya kupikia, kuanzisha vitalu vya kuzalisha mbegu bora za mafuta ya kula na kuanzisha mashamba makubwa ya kulima alizeti na ngano,”alisema Prof. Mkumbo.

Alisema sekta nyingine ni ufugaji kwa kuanzisha malisho ya mifugo, ranchi za biashara, uvuvi na ufugaji wa Samaki na kuanzisha viwanda vya kuchakata Samaki, utalii, ujenzi wa majengo kwa kujenga nyumba za makazi, ofisi, kumbi za mikutano, Madini, Huduma za fedha, Misitu, Nishati (ikiwemo mafuta na gesi).

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.