MTAALA MPYA ELIMU KUWAWEZESHA VIJANA KUJIAJIRI NA KUAJIRIWA:PROF.MKENDA.
Na.Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imetangaza kuwa mtaala mpya wa elimu utakaoanza kutumika mwaka 2028 utalenga kuwawezesha vijana kuajiriwa na kujiajiri wanapomaliza sekondari ambapo Mtaala huo utaweka elimu ya lazima hadi sekondari, ambapo shule ya msingi itahitimishwa darasa la sita badala ya saba, hatua inayolenga kuendana na mahitaji ya sasa ya soko la ajira.
Hayo yamesemwa leo Disemba 10,2025 Jijini Dar es salaam na waziri Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda, amesema kuwa mageuzi haya ni utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya elimu iwe ya kizazi kipya na inayotoa ujuzi wa moja kwa moja huku akibainisha kuwa mtaala mpya unatoa mikondo miwili ya elimu ya sekondari: elimu ya jumla na elimu ya amali, ambayo inalenga kuongeza ujuzi wa vitendo.
"Katika mfumo mpya, mwanafunzi atamaliza darasa la sita na kuendelea na sekondari ya kati kwa miaka minne. Elimu ya sekondari itawafanya wanafunzi kupata ujuzi wa msingi unaowawezesha kuingia kwenye ajira au kuendelea na masomo ya juu. Prof. Mkenda alisema mfumo wa sasa wa 7+4+3+2 utaondolewa na kubadilishwa na mfumo wa 6+4+2 au 3+3 kulingana na mkondo wa masomo",Amesema.
Alifafanua kuwa elimu ya amali itatoa ujuzi wa ufundi na ufundi stadi, na mwanafunzi atakapohitimu kidato cha nne atapata cheti cha VETA pamoja na cha sekondari, hatua itakayomuwezesha kuajiriwa moja kwa moja. Pia serikali inaendelea kujenga shule 103 za ufundi kote nchini ili kuimarisha utoaji wa mafunzo hayo.
Aidha, Prof. Mkenda alisema kwamba somo la biashara, historia ya Tanzania na maadili vitakuwa vya lazima katika sekondari, huku Kiingereza kikifundishwa kuanzia darasa la kwanza hadi la sita, na Kiswahili pia kwa shule zenye mchepuo wa Kiingereza. Alisisitiza kuwa mageuzi haya yanalenga kupunguza changamoto zilizopo kwenye mfumo wa sasa na kuwafanya vijana kuwa tayari zaidi kuingia katika maisha ya uzalishaji na ajira.
Waziri alisema Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi chache zilizoendelea kubaki na elimu ya lazima chini ya miaka tisa, jambo lililoonekana kurudisha nyuma maendeleo. Mageuzi haya yatasaidia kupanua wigo wa vijana wanaomaliza msingi kuendelea na sekondari, ambapo zaidi ya asilimia 75 ya wanafunzi wa sasa tayari wanaendelea na masomo ya sekondari.
Alibainisha kuwa serikali imejipanga kupokea idadi kubwa ya wanafunzi watakaohitimu darasa la sita kwa wakati mmoja na kuingia sekondari mwaka 2027. Pia alisema umri wa kuanza shule ukiwa miaka sita, watoto hitimu wakiwa na miaka 13, na bila mfumo mpya isingekuwa rahisi kwao kuajiriwa au kujiajiri.
Prof. Mkenda alisisitiza kuwa mageuzi ya elimu ni muhimu kwa mustakabali wa taifa na yataifanya sekta ya elimu kuakisi mahitaji halisi ya kizazi kipya, kuongeza ubora wa elimu na kujenga msingi wa uchumi wa viwanda na maarifa.



Comments
Post a Comment