NDEJEMBI AIPONGEZA TANESCO KWA KUZINDUA MITA JANJA.
Na Sophia Kingimali.DAR ES SALAAM
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kufanya mageuzi makubwa ya kiteknolojia kwenye sekta ya nishati, wakati akizindua rasmi Mita Janja (Smart Meters) za TANESCO, mfumo wa kisasa unaolenga kuongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa watumiaji wa umeme kote nchini.
Akizungumza katika hafla hiyo leo Disemba 5,2025 Jijini Dar es salaam Waziri Ndejembi amesema hatua hiyo ni ya kihistoria kwa TANESCO katika kuimarisha utoaji wa huduma.
"Uzinduzi huu ni tukio muhimu na la kimapinduzi katika mageuzi ya kidigitali ya shirika Serikali imejipambanua kuboresha upatikanaji wa umeme bora unaoendana na matakwa ya karne ya 21 niipongeze TANESCO kwa kuwa miongoni mwa mashirika ya umma yanayofanya vizuri kwenye huduma kwa wananchi, hatua inayodhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan",Amesema.
Waziri Ndejembi amesema Mita Janja zimebuniwa kuondoa changamoto nyingi zilizokuwepo kwenye mita za zamani, ikiwemo hitilafu za tokeni kutokuingia, kupotea kwa kumbukumbu, na rimoti kuharibika kirahisi. Amesema wateja wengi walipata usumbufu kutokana na mita kuwekwa maeneo magumu kufikiwa na hivyo kulazimika kupanda ngazi au viti kila wanapotaka kuingiza tokeni.
"Kwa muda mrefu, wateja walikosa uwezo wa kufuatilia matumizi ya umeme kwa wakati halisi, jambo lililowafanya wengi kushindwa kupanga bajeti zao ipasavyo hizi Mita Janja zinakuja kama suluhisho la kudumu, kwani zinaonyesha matumizi sekunde kwa sekunde na kutoa taarifa pale umeme unapoanza kuisha",Amesema.
Aidha, ameeleza kuwa malalamiko kuhusu rimoti zilizokuwa zikivunjika, kuvuja betri, au kushindwa kuingiza tokeni yamekuwa yakisababisha usumbufu mkubwa hasa wakati wa dharura. Teknolojia hii mpya, amesema, imeondoa kabisa utegemezi wa rimoti na inawezesha mteja kuingiza umeme popote alipo kwa kutumia mfumo wa kisasa.
Waziri amesema manufaa ya Mita Janja si kwa wateja pekee, bali hata kwa TANESCO, kwani zina uwezo wa kugundua wizi wa umeme, kubaini uharibifu wa mita, pamoja na kutambua upotevu wa nishati kwa wakati halisi—jambo litakaloimarisha mapato ya shirika na kulinda fedha za Serikali. Tayari utekelezaji wa awali umeanza katika mikoa mbalimbali na wateja wameonyesha kufurahia maboresho hayo.
Amesema TANESCO imekuwa ikiwekeza kwenye teknolojia za kisasa ikiwemo mfumo wa Nikonekt kwa maombi ya kuunganishiwa umeme, kituo cha kisasa cha kupokea miito ya wateja (Unified Call Centre), na Chatbot ya JISOti inayowawezesha wateja kujihudumia bila kusubiri mawasiliano ya moja kwa moja.
Akitoa maelekezo kwa TANESCO, Waziri Ndejembi amelitaka shirika hilo kuharakisha usambazaji wa Mita Janja kwa wateja wa maeneo yote yenye uhitaji mkubwa bila gharama, sambamba na kuhakikisha kuwa wateja wapya wote wanachomekewa mita hizo ili kupunguza utegemezi wa mita za zamani. Hata hivyo, amesema kubadilisha zaidi ya mita milioni 5.6 zilizopo nchini si kazi ya siku moja, hivyo utafanyika kwa awamu.
"Usalama, ubora na viwango vya kimataifa lazima vizingatiwe, huku elimu kwa umma ikitolewa kwa kina ili kila mteja aelewe matumizi ya mfumo huu mpya niwaagize TANESCO mfumo wa AMI unaoendesha mita hizo ubadilishwe na kuboreshwa kila mwaka kuendana na kasi ya maendeleo ya teknolojia",amesema.
Waziri ameongeza kuwa uwajibikaji unatakiwa kupewa kipaumbele, huku ubunifu na mawasiliano endelevu na wateja yakiboreshwa zaidi ili kuimarisha utoaji wa huduma bora hivyo ameitaka TANESCO kuendelea kuonesha mfano mzuri kwa mashirika mengine ya umma.
Amesema Serikali itaendelea kufuatilia utekelezaji wa mradi huo hadi Tanzania iwe na mfumo kamili wa usimamizi wa umeme wa kisasa na wenye tija. Amewapongeza wataalamu wa ndani wa TANESCO kwa kuendeleza mradi huu kwa miaka 18 bila kutegemea utaalam wa nje pekee, akisema wameweka historia mpya kwenye sekta ya umeme.
Waziri pia amewapongeza wadau wa ndani na nje kwa kutoa mchango wao katika utafiti, majaribio na uwekezaji wa mita hizo, akisema mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano thabiti ambao unaendelea kuiletea nchi manufaa makubwa katika mapinduzi ya kiuchumi na kiteknolojia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange amesema mabadiliko ya kidijitali yanayoendelea ndani ya Shirika yamekuwa na mafanikio na kuongeza ufanisi katika utendaji wa Shirika huku akiita uzinduzi wa mita janja “game changer”.






Comments
Post a Comment