SERIKALI KUANZISHA KITUO MAALUM KUWAWEZESHA WAWEKEZAJI VIJANA.
Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
Serikali inatarajia kuanzisha kituo Maalum cha kuhudumia na kuwezesha wawekezaji vijana(Youth Investors Resource Centre) nchini lengo likiwa kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira na kuongeza fursa za uwekezaji kwa vijana,
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 8,2025 jijini Dar es Salaam, uliolenga kutoa mwelekeo wa kisera na kiutendaji wa Serikali kupitia Wizara ya Mipango na Uwekezaji kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesema katika kipindi cha miaka mitano ijayo, seriakli itaanzisha programu maalum ya kuwezesha wawekezaji vijana kubuni na kuanzisha uwekezaji wa viwanda nchini kote.
“Kwa kuanzia, tutatenga maeneo ambayo vijana waliomaliza vyuo vikuu na vyuo vya ufundi watapewa ili kuweza kuwekeza kwenye viwanda,”alisema.
Amesema Programu hiyo itahusisha mafunzo, uwezeshaji wa kupewa ardhi, kuunganishwa na wauzaji wa mitambo na malighafi (machinery and raw materials), na pia kuunganisha na benki ambazo zina ushirikiano na TISEZA ikiwemo Benki ya Azania, TCB, na CRDB.
“Tunatenga maeneo maalum kwa uwekezaji utakaofanywa na vijana Dodoma Nala lenye Ekari 100), Pwani eneo la Kwala lenye Ekari 20, Mara kule Bunda lenye Ekari 100), Ruvuma Songea lenye Ekari 100 na Bagamoyo Pwani kuna Ekari 20,”alisema.
Amesema programu hiyo itaizinduliwa pamoja na Kituo Cha Kuwezesha Vijana kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Prof Mkumbo ameongeza kuwa serikali inakusudia kusogeza huduma za Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi kufikia kila Mkoa ifikapo mwaka 2028.
“Kila Mkoa utakuwa na kituo maalum cha kutangaza na kuwezesha wawekezaji sambamba na agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kusogeza huduma kwa wananchi wote.
“Tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI kuratibu na kuwezesha huduma hizi kuwafikia wote nchini,”alisema.
Amesema kwa kushirikiana na sekta binafsi, kutajengwa miundombinu ya uwekezaji wa viwanda nchi nzima.
“Kwenye eneo hili, TISEZA itaingia ubia na wenye mitaji ili kujenga industria shades ambazo zitakodishwa kwa gharama nafuu kwa mtanzania yeyote anayetaka kuwekeza kwenye viwanda.
“Mpango huu utapunguza gharama za watanzania kuwekeza na kunufaika na mageuzi ya kiuchumi yanayotokea nchini kote. Hatua hii itaongeza fursa za kiuchumi na kukuza kipato cha mtanzania mmoja mmoja,”alisema.
Amesema serikali itabuni na kuanzisha vivutio vipya vya kiuwekezaji mara kwa mara ili kuongeza uimara wa uwekezaji nchini na mvuto wa Tanzania kwa wote wenye mitaji huko duniani
Amesema katika kuendelea kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, Serikali inakamilisha maandalizi ya mkakati mpya wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini (MKUMBI II) utakaozinduliwa kabla ya kuanza utekelezaji wa Dira 2050 hapo Julai 1,2026.




Comments
Post a Comment