VIONGOZI WA DINI WAASWA KUTUMIA STAHA KWENYE KUKEMEA MAOVU.

 


Na.Sophia Kingimali.


Muumini wa Kanisa Katoliki, Mwalimu Ludovick Joseph, amesema viongozi wa dini wana haki na wajibu wa kiroho kukemea maovu yanapotokea katika jamii ili kujenga dhamiri za waumini na kutoa mwelekeo wa kimaadili kwa Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Disemba 30,2025 katika tafakari yake kwa umma, Mwalimu Ludovick amesema kauli za viongozi wa dini kuhusu masuala nyeti ya kijamii na kitaifa ni halali, kwani zina mchango mkubwa katika kuhimiza haki, amani na maadili mema miongoni mwa waumini na jamii kwa ujumla.

Hata hivyo, amesema kasoro kubwa inayojitokeza ni matumizi ya lugha, akisisitiza kuwa uongeaji wa viongozi wa dini haupaswi kufanana na lugha ya wanasiasa au wapinzani wa kisiasa, bali uwe wa kidini, kichungaji na wa kimaadili.

Amefafanua kuwa viongozi wa dini wanapaswa kutumia lugha ya upendo, maridhiano na hekima, huku wakiepuka kauli zinazoweza kuchochea migawanyiko au kuleta taharuki katika jamii.

Pia amekosoa wingi wa matamko kutoka kwa viongozi wa dini kwa muda mfupi, akisema si vyema kiongozi wa dini kutoa tamko leo, kesho na kesho kutwa, bali ni muhimu kutoa nafasi kwa waumini na jamii kufanya tafakari ya kina juu ya ujumbe uliotolewa.

"Nitoe wito kwa viongozi wa dini kuendelea kukemea maovu na kujenga dhamiri za waumini, lakini wafanye hivyo katika mstari wa maridhiano, upendo na kusaidiana, ili kulijenga taifa lenye umoja na mshikamano kama ilivyokuwa hapo awali",Amesema Mwalimu Ludovick.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.