WAJASILIAMALI DSM WALAANI MAANDAMANO NA VURUGU WAAHIDI KUSHIRIKI KWENYE ULINZI WA AMANI.

 


Na.Mwandishi wetu

Wajasiriamali wa mkoa wa Dar es Salaam wamelaani vikali maandamano na vurugu za Oktoba 29, wakisisitiza kuwa vitendo hivyo vimeathiri kwa kiasi kikubwa biashara zao, ajira na ustawi wa jamii, huku wakitangaza kujipanga kulinda amani na mshikamano wa taifa.

Tamko hilo limetolewa leo jijini Dar es Salaam na wawakilishi wa wafanyabiashara kutoka wilaya zote tano za mkoa huo ambazo ni Ilala, Temeke, Ubungo, Kinondoni na Kigamboni, mbele ya waandishi wa habari, wakisema amani ndiyo msingi wa maendeleo na uchumi wa huduma unaotegemewa na wakazi wa jiji hilo.

Akizungumza kwa niaba ya wajasiriamali wa Ilala, Selemani, mfanyabiashara wa vifaa vya michezo kutoka Mboto, alisema kuwa bila amani hakuna biashara, hakuna ajira na hakuna maendeleo, hivyo kundi hilo limeazimia kupaza sauti kupinga vurugu na uchochezi wa aina yoyote.

Selemani aliongeza kuwa wajasiriamali wanapinga vikali watu wanaohamasisha machafuko wakiwa nje ya nchi au kupitia mitandao ya kijamii, akisema mara nyingi wao hawabebi madhara ya vitendo hivyo, wakati wananchi wa kawaida ndio huathirika moja kwa moja.

Kwa upande wake mwakilishi wa Temeke alisema kuwa vurugu hizo zilisababisha uharibifu wa miundombinu ikiwemo vituo vya mwendokasi, kukosekana kwa huduma za usafiri na kupotea kwa ajira na vyanzo vya kipato kwa wananchi wengi, hali iliyoacha mzigo mkubwa wa kiuchumi kwa jamii.

Alisema serikali inalazimika kutumia kodi za wananchi kurejesha miundombinu iliyoharibiwa, jambo ambalo lingeweza kuepukika endapo amani ingelindwa, hivyo akatoa wito kwa wote kukataa kushawishika kuingia katika machafuko yanayodhoofisha taifa.

Mwakilishi wa Ubungo, Hussein Bambe kutoka Kimara, alisema wafanyabiashara wadogo wamejifunza kuwa machafuko si njia sahihi ya kuleta mabadiliko ya kisiasa, kwani waathirika wakubwa huwa ni wananchi wa hali ya chini wanaopoteza mitaji yao iliyojengwa kwa miaka mingi.

Bambe alieleza kuwa baada ya vurugu hizo, hali ya ulinzi na huduma muhimu ilidorora katika baadhi ya maeneo, hali iliyowafanya wafanyabiashara kufanya kazi kwa hofu, akisisitiza kuwa umoja wa wafanyabiashara ni muhimu ili kulinda maslahi yao na jamii kwa ujumla.

Naye Waperejea Michael, machinga kutoka Kinondoni anayefanya biashara katika soko la Makumbusho, alisema machinga wamekuwa waathirika wakubwa wa vurugu, akionya dhidi ya wanasiasa na watu wanaotumia mitandao kueneza chuki, migawanyiko na uchochezi kwa maslahi binafsi.

Aliongeza kuwa wajasiriamali wanakemea pia viongozi wa dini wanaotumia majukwaa yao kuchochea vurugu au migawanyiko, akisema vitendo hivyo vinahatarisha mshikamano wa kitaifa na amani iliyojengwa kwa muda mrefu.

Kwa upande wake mzee Omar Abubakar Ilunga, mfanyabiashara mkongwe wa Kariakoo, alisema vurugu za Oktoba 29 zilisababisha wananchi wengi kujifungia majumbani kwa hofu, kukosa huduma muhimu na kuathiri maisha ya kila siku, akisisitiza kuwa hayo ni mafunzo kwa Watanzania wote kulinda amani.

Mzee Ilunga alisisitiza kauli mbiu ya “Tanzania ni mimi,” akimaanisha kuwa kila raia ana wajibu wa kulinda nchi, uchumi na miundombinu, bila kujali nani yuko madarakani, kwani viongozi hubadilika lakini taifa hubaki.

Katika maazimio yao, wajasiriamali wamekubaliana kupinga vurugu, uchochezi, uharibifu wa mali za umma na binafsi, pamoja na matusi ya kisiasa, na badala yake kuchagua amani kama njia pekee ya kulinda maisha, biashara na mustakabali wa taifa.

Wameahidi kushirikiana na taasisi mbalimbali na kutembelea masoko na vijiwe katika wilaya zote tano ili kueneza ujumbe wa amani, wakitoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote kuungana, kukataa vishawishi vya machafuko na kulinda ustawi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.