Waumini wa Kanisa Katoliki watoa tamko dhidi ya kauli za Askofu Rwaichi.
Na Mwandishi Wetu.
Waumini wa Kanisa Katoliki, McDonald Silinde na Gerald Abel, wametoa tamko kwa vyombo vya habari wakilaani kauli walizodai zilitolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Jude Thaddeus Ruwa’ichi, wakati wa mahubiri ya Misa ya Krismasi iliyofanyika Desemba 25, 2025.
Akisoma tamko hilo mbele ya waandishi wa habari leo Disemba 27,2025 Jijini Dar es Salaam, MacDonald Silinde amesema wametoa tamko hilo kwa huzuni na masikitiko makubwa, wakieleza kuwa maneno yaliyotamkwa madhabahuni yamewaumiza waumini wengi kisaikolojia na kiimani, na kuvunja misingi ya mafundisho ya Kikristo.
Silinde amesisitiza kuwa madhabahu ya kanisa ni mahali patakatifu pa kuhubiri Neno la Mungu, kuimarisha imani na kuleta faraja, na si jukwaa la matusi, vitisho au lugha ya chuki dhidi ya waumini.
Kwa mujibu wao, maneno makali na ya kudhalilisha yaliyodaiwa kutumiwa na Askofu, yakiwataja waumini kwa misemo kama “wapumbavu” na “wasaliti”, hayana nafasi katika mahubiri ya Kikristo yanayopaswa kuongozwa na upendo, haki na neema.
Aidha Silinde alinukuu maandiko ya Biblia yakisisitiza wajibu wa viongozi wa kiroho kuwa wajenzi wa amani na umoja, wakirejea Mathayo 5:9 na Wakolosai 4:6, wakisema neno la kiongozi wa kanisa linapaswa kujenga na kutia moyo, si kubomoa.
Waumini hao pia walikumbusha neno kutoka kitabu cha Mathayo 18:15 linaloelekeza kwamba pale panapokuwa na kosa, maonyo yafanyike faraghani, na si kuburuzana hadharani madhabahuni, jambo walilodai linawakwaza na kuwavunja moyo waumini.
Kuhusu chanzo cha mjadala, amesema bado hakuna majibu ya wazi kuhusu hoja zilizowasilishwa katika barua iliyofikishwa kwa Balozi wa Vatican nchini na waumini wenzao, wakidai badala ya kujibiwa, waumini waliotoa hoja hizo walijibiwa kwa matusi.
Aidha Katika tamko lao, wameeleza wasiwasi kuhusu madai ya kuingizwa kwa kanisa katika siasa za chama kimoja, wakimtaja Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima, na kudai suala hilo linapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kina.
Silinde amesisitiza kuwa zama za viongozi wa dini kutisha waumini na kujiona hawakosei zimepitwa na wakati, wakisema kanisa la leo linahitaji viongozi wanaosikiliza, kuheshimu dhamira za waumini na kutambua kuwa kanisa linajengwa na waumini wote.
Amefafanua kuwa padri au askofu si kanisa, bali kanisa ni waumini, na kwamba kiongozi wa kiroho anapaswa kuwa muunganisha wa jamii, si chanzo cha migawanyiko, huku wakiongeza kuwa imani ya Kikristo si utaifa wala mali ya mtu yeyote.
Waumini hao wametangaza kuunga mkono kikamilifu waumini wenzao waliowasilisha barua Vatican, na kueleza kuwa wao pia watawasilisha malalamiko rasmi dhidi ya Padri Kitima na Askofu Ruwa’ichi,
"lengo letu ni kulinda heshima na taswira ya Kanisa Katoliki kwani kanisa ni kubwa kuliko mtu au cheo chochote,hivyo linapaswa kujengwa na misingi ya upendo, haki, umoja na mshikamano, si kwa matusi, hukumu, hofu wala upendeleo wa kisiasa hivyo tunatoa wito kwa viongozi wa kanisa kurejea misingi hiyo",Amesema


Comments
Post a Comment