DCEA YATOA RAI KWA WANANCHI KUWA MAKINI NA MIZIGO WANAYOSAFIRISHA BILA KUJUA KILICHOBEBWA.
Na.Sophia Kingimali.
Mamlaka ya kudhibiti na kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini (DCEA) imetoa wito kwa wananchi kutojihusisha na kusafirisha vifurushi au mizigo wasiyoifahamu, pamoja na kutoa taarifa mapema wanapohisi viashiria vya uvunjifu wa sheria, huku ikisisitiza kuwa itaendelea na operesheni kali nchi nzima dhidi ya wahusika wa biashara hiyo haramu.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya operesheni zilizofanyika mwezi Desemba 2025,leo Januari 8,2026, Kamishina Jenerali Aretas Lyimo amesema kuwa jumla ya kiasi kikubwa cha dawa za kulevya chenye uzito wa zaidi ya kilogramu 9,683.89 kilikamatwa katika mikoa mbalimbali, huku watuhumiwa kadhaa wakikamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Amesema katika tukio la jijini Dar es Salaam, raia wa Kenya, Kilonzo Mwende (35), alikamatwa katika mtaa wa Bustani, Sinza, akiwa na gramu 131 za heroin. Uchunguzi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akiishi nchini tangu mwaka 2023 akijifanya mfanyabiashara wa kuuza chai ya maziwa katika ofisi mbalimbali, huku akitumia shughuli hiyo kama kifuniko cha kusambaza dawa za kulevya.
Amesema mtuhumiwa huyo amekiri kuanza kuingiza dawa za kulevya kidogo kidogo baada ya kubaini upungufu wa dawa hizo nchini, akizisambaza katika maeneo mbalimbali ya jiji ili kujipatia kipato, hali iliyoibua wito kwa wananchi kutoa taarifa kuhusu wageni au biashara zinazotia shaka katika maeneo yao kupitia namba maalum ya dharura 119.
Aidha, watuhumiwa wawili, Amani Idi Mrisho (40), mkazi wa Buza Dar es Salaam, na Selemani Juma Ally (32), raia wa Msumbiji, walikamatwa kuhusiana na usafirishaji wa dawa za kulevya kwa kutumia basi la abiria aina ya King Masai Tours lililokuwa likifanya safari kati ya Msumbiji na Tanzania.
"Uchunguzi umebaini kuwa basi hilo lilifanyiwa mabadiliko kinyume cha sheria kwa kung’oa baadhi ya viti vya abiria na kutengeneza maficho ya siri kwa ajili ya kubeba mizigo haramu, ikiwemo dawa za kulevya, hali iliyoibua tahadhari kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri dhidi ya kufanyiwa “modification” bila uangalizi",Amesema.
Aidha Kamishna Jenerali Lyimo alibainisha kuwa mbinu kama hizo zinatumika kwenye malori, ambapo hutengenezwa maficho katika kichwa cha dereva, bodi au chesisi kwa ajili ya kusafirisha dawa za kulevya, na kusisitiza kuwa mmiliki wa chombo cha usafiri atawajibika kisheria endapo gari lake litabainika kutumika katika uhalifu huo.
Amesema Katika operesheni nyingine, watu watatu walikamatwa wakiwa wanasafirisha bangi yenye uzito wa zaidi ya kilogramu 1,893 kutoka mkoani Morogoro kwenda Dar es Salaam, huku mamlaka ikionya pia kuhusu matumizi ya baadhi ya watumishi wa serikali kama vichaka vya kupitisha dawa hizo kwa kutumia vitambulisho vya kazi.
Aidha, katika ukaguzi wa kampuni za usafirishaji mizigo jijini Dar es Salaam, amesema pakiti za mirungi zenye uzito wa kilogramu 9.54 zilikamatwa zikiwa zimefichwa na kusomeshwa kama majani ya mwarobaini, zikitokea nchini Kenya, huku operesheni zilizofanyika katika mikoa mbalimbali zikikamata heroin, bangi na mirungi kwa kiasi kikubwa pamoja na kuteketeza hekari 14 za mashamba ya bangi.
"Mamlaka inasisitiza kuwa itaendelea kuimarisha operesheni hadi ngazi ya wilaya na vijiji, kudhibiti uzalishaji na usafirishaji wa bangi na mirungi, na kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa ili kuvunja na kumaliza kabisa mitandao ya biashara ya dawa za kulevya nchini Tanzania",Amesema Kamishna Jenerali Lyimo.



Comments
Post a Comment