NECTA YAIPONGEZA SERIKALI KWA KULETA MAGEUZI SEKTA YA ELIMU
Na. Sophia Kingimali.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA)Profesa Said Mohammed,amesema kuwa juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimeleta mageuzi makubwa katika sekta ya elimu, hususan katika kuimarisha stadi za msingi za KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu) kwa wanafunzi wa elimu ya awali na msingi.
Akizungumza leo Januari 29,2026 Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango Mkakati wa kisayansi wa kujenga umahiri wa kusoma,kuandika na kuhesabu KKK, kwa wanafunzi wa awali,darasa la kwanza na la pili amesema tukio hilo ni la kihistoria na linaonesha dhamira ya dhati ya Rais katika kuboresha elimu nchini.
Ameeleza kuwa mpango wa KKK unalenga watoto wa miaka mitano hadi saba, ambao ni umri wa msingi katika kujenga uwezo wa kujifunza.
"Endapo mtoto hatapata stadi hizo mapema, huathirika katika nyanja zote za ukuaji ikiwemo kiakili, kijamii na kihisia. Kwani hali hiyo ni sawa na mtoto mchanga anayekosa maziwa ya mama, KKK ni msingi wa elimu ya baadaye",Amesema.
Katibu Mtendaji huyo amebainisha kuwa tangu mwaka 2015 NECTA imekuwa ikifanya upimaji wa kitaifa kwa sampuli, na matokeo yalionesha kuwa kati ya asilimia 67 hadi 87 ya wanafunzi walikuwa na umahiri wa KKK, huku changamoto kubwa zikiwa katika kusoma kwa ufasaha, kuandika kwa usahihi na kuhesabu.
"Mafunzo yaliyotolewa kwa walimu na maboresho ya mazingira ya ujifunzaji yamechangia kupungua kwa idadi ya wanafunzi wasio na stadi hizo",Amesema katibu...
Aidha, amesema kwa mara ya kwanza mwaka 2025 NECTA ilifanya upimaji wa kitaifa wa darasa la pili ngazi ya shule, uliowahusisha wanafunzi zaidi ya milioni 1.7 katika shule zaidi ya elfu 8, kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa PRN. Hatua hiyo imelenga kutambua mapema changamoto za wanafunzi ili zichukuliwe hatua kabla hawajafika madarasa ya juu.
Kwa upande wa ufaulu wa masomo ya sayansi na hisabati, Katibu Mtendaji amesema takwimu zinaonesha kuimarika kwa matokeo, hususan katika somo la Advanced Mathematics kwa kidato cha sita, ambapo ufaulu umefikia karibu asilimia 100 katika miaka ya karibuni.
Amesisitiza kuwa wadau wa elimu wanapaswa kutumia njia za kisayansi kutatua changamoto zilizopo, ikiwemo kuondoa hofu ya hisabati (numerophobia) na kuboresha mbinu za ufundishaji ili kuongeza ari ya wanafunzi.





Comments
Post a Comment