RAIS DKT. SAMIA AZINDUA MPANGO MKAKATI WA KKK AWATAKA WAANGALIZI WA ELIMU NCHINI KUSIMAMIA UTEKELEZAJI WAKE.
Na Sophia Kingimali-Dar es salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa waangalizi wa elimu nchini kusimamia kwa karibu utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kisayansi wa Kujenga Umahiri wa Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK),huku akisisitiza kuwa mpango huo usibaki kwenye makaratasi bali utoe matokeo halisi kwa watoto wa awali pamoja na wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili.
Wito huo ameutoa leo Januari 29,2026 wakati wa uzinduzi wa mpango huo jijini Dar es Salaam, Rais Samia ame sema lengo kuu la mkakati huo ni kuhakikisha hakuna mtoto anayefika darasa la tatu bila kuwa na uwezo wa msingi wa kusoma, kuandika na kuhesabu, kwani stadi hizo ndizo msingi wa mafanikio ya masomo katika ngazi zote za elimu.
Aidha Rais Samia ameipongeza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI pamoja na wadau wa maendeleo kwa maandalizi ya mpango huo, akisema jitihada hizo zinaonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kuboresha ubora wa elimu nchini.
Ameeleza kuwa mpango mkakati huo ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi zake za siku 100 pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga taifa linaloongozwa na maarifa, sayansi na teknolojia kwa maendeleo endelevu.
"Mtoto anayejengewa umahiri wa KKK mapema huwa na uwezo mkubwa wa kufikiri kwa kina, kuelewa maarifa mapya na kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kujifunza, hali inayochangia kukuza rasilimali watu bora kwa taifa",Amesema Dkt.Samia.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia na vifaa vya kufundishia vinavyotengenezwa ndani ya nchi, kwani vimebuniwa kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania na vina uwezo wa kumsaidia mtoto kujifunza kwa vitendo na kwa urahisi zaidi.
Katika hotuba yake, Rais Samia pia alieleza jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu, ikiwemo ujenzi wa madarasa na ajira ya walimu, huku akisisitiza kuwa pamoja na uwekezaji huo, ubora wa ufundishaji na ufuatiliaji wa karibu wa wakaguzi wa elimu ni jambo la msingi.
Aidha Dkt Samia ametoa wito kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mpango huo, akisema mafanikio ya elimu ya watoto si jukumu la Serikali pekee bali ni wajibu wa kila mwananchi kwa ustawi wa taifa.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda amesema mpango huo unalenga kuimarisha ubora wa elimu kupitia mafunzo endelevu kwa walimu, maandalizi ya vifaa bora vya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kushirikisha walimu katika kubuni mbinu rahisi na bunifu za ufundishaji ,huku akieleza kuwa nyenzo hizo zitapatikana kirahisi katika maeneo yote ya nchi, zikiwemo zinazotengenezwa kwa malighafi za ndani, ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata fursa sawa ya kujifunza.
Aidha, amesisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo utafanyika kwa kipindi cha miaka mitano kwa ushirikiano na TAMISEMI na taasisi nyingine za elimu, huku Serikali ikiahidi kutoa mrejesho wa kila mwaka kuhusu hatua zilizofikiwa. Prof. Mkenda alitoa wito kwa wadau wa elimu kushirikiana kikamilifu ili kuhakikisha matokeo chanya yanaonekana kwa vitendo, akibainisha kuwa lengo kuu ni kuboresha msingi wa elimu na kuongeza umahiri wa wanafunzi nchini.
Naye Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA),Said Mohamed Ameeleza kuwa mpango wa KKK unalenga watoto wa miaka mitano hadi saba, ambao ni umri wa msingi katika kujenga uwezo wa kujifunza,kwani endapo mtoto hatapata stadi hizo mapema, huathirika katika nyanja zote za ukuaji ikiwemo kiakili, kijamii na kihisia.
Aidha, amesema kwa mara ya kwanza mwaka 2025 NECTA ilifanya upimaji wa kitaifa wa darasa la pili ngazi ya shule, uliowahusisha wanafunzi zaidi ya milioni 1.7 katika shule zaidi ya elfu 8, kwa kutumia mfumo wa kidijitali wa PRN. Hatua hiyo imelenga kutambua mapema changamoto za wanafunzi ili zichukuliwe hatua kabla hawajafika madarasa ya juu.






Comments
Post a Comment