Tutuba: Benki Kuu Yabakiza Riba Asilimia 5.75, Uchumi Waendelea Kuwa Imara.
Na.Mwandishi wetu.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba, amesema kuwa Riba ya Benki Kuu (CBR) imebakizwa kuwa asilimia 5.75 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2026, huku akieleza kuwa uamuzi huo unalenga kuendeleza utulivu wa uchumi na kuchagiza ukuaji endelevu wa shughuli za kiuchumi nchini.
Akizungumza leo Januari 8,2026 Jijini Dar es salaam kufuatia kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) kilichofanyika tarehe 7 Januari 2026, Tutuba amesema uamuzi wa kubakiza riba umetokana na mwenendo mzuri wa mfumuko wa bei unaotarajiwa kuendelea kubaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.
"Hatua hiyo itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ukuaji wa uchumi, ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa sekta binafsi na kuendeleza uthabiti wa mfumo wa fedha nchini",Amesema.
Aidha Gavana ameongeza kuwa Benki Kuu itaendelea kutekeleza sera ya fedha kwa kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki (7-day interbank rate) inabaki ndani ya wigo wa asilimia 3.75 hadi 7.75, hatua inayolenga kudhibiti ukwasi na kuimarisha utulivu wa soko la fedha.
Akielezea hali ya uchumi wa dunia, Tutuba amesema uchumi wa kimataifa uliendelea kuimarika kwa kasi ya kuridhisha mwaka 2025 licha ya changamoto za migogoro ya kisiasa, ongezeko la ushuru wa forodha na kutokutabirika kwa matarajio ya kiuchumi. IMF inakadiria uchumi wa dunia kukua kwa asilimia 3.2 mwaka 2025 na kuendelea kukua kwa kasi hiyo mwaka 2026.
Ameongeza kuwa mfumuko wa bei duniani umeendelea kupungua katika nchi nyingi kutokana na kushuka kwa bei za nishati na utekelezaji wa sera madhubuti za fedha, hali inayotarajiwa kusaidia mfumuko wa bei nchini kuendelea kubaki ndani ya lengo kwa mwaka 2026.
Kuhusu bei za bidhaa za kimataifa, Gavana Tutuba amesema bei ya mafuta ghafi ilishuka hadi kati ya dola 62 na 65 kwa pipa katika robo ya nne ya 2025, hali inayosaidia kupunguza gharama za uagizaji na kuimarisha utulivu wa thamani ya shilingi huku bei ya dhahabu duniani ikitarajiwa kuongeza mapato ya fedha za kigeni kupitia mauzo ya madini.
Akizungumzia Kwa upande wa uchumi wa ndani, Tutuba ameeleza kuwa uchumi wa Tanzania Bara ulikua kwa kasi ya takriban asilimia 5.9 mwaka 2025, ukichangiwa zaidi na sekta za kilimo, madini na ujenzi, huku uchumi wa Zanzibar ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.8 mwaka 2026 kutokana na ujenzi, utalii na uzalishaji viwandani.
Amesema mfumuko wa bei uliendelea kuwa tulivu, ukiwa wastani wa asilimia 3.5 Tanzania Bara na asilimia 3.4 Zanzibar katika robo ya nne ya 2025 huku Sekta ya benki nayo ikiendelea kuwa imara, huku uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) ukishuka hadi asilimia 3.1 na akiba ya fedha za kigeni kufikia zaidi ya dola bilioni 6.3.
Gavana Emmanuel M. Tutuba amesema Kamati ya Sera ya Fedha inatarajia kukutana tena tarehe 2 Aprili 2026, huku tangazo la Riba ya Benki Kuu kwa robo ya pili ya mwaka litafanyika tarehe 3 Aprili 2026.





Comments
Post a Comment