WAZEE DAR WAWATAKA GEN Z KUDUMISHA AMANI, WAMPONGEZA RAIS SAMIA SIKU YA KUMBUKIZI YA KUZALIWA
Na Mwandishi Wetu.
Baadha ya Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam wametoa wito mzito kwa vijana wa kizazi cha Gen Z kudumisha upendo na amani, wakisema kuwa hiyo ndiyo misingi ya maendeleo ya Taifa,
Wito huo wameutoa leo Januari 27,2026 Jijini Dar es salaam wakati wa hafla ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, iliyoandaliwa na taasisi ya Vijana innovation na kuratibiwa na taasisi ya Together for Samia.
Wazee hao wamesema kuwa Tanzania imebarikiwa amani kubwa inayotamaniwa na mataifa mengi, hivyo vijana wanapaswa kuwa walinzi wakuu wa tunu hiyo kwa kuishi kwa upendo, mshikamano na kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi.
Akizungumza kwa niaba ya wazee, bi Sophia amesema kuwa wao kama wazee wataendelea kuliombea Taifa, lakini vijana nao wana wajibu wa kuhakikisha amani inatawala kwa vitendo, kwani bila amani hakuna maendeleo wala ustawi wa kweli.
“Ni nchi ya amani, tusivuruge amani tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Amani hii inatafutwa na nchi nyingine. Vijana, tusaidieni kuilinda na kuikuza,” amesema mzee huyo huku akiwataka vijana kujishughulisha na kazi na kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa.
Sambamba na hayo, wazee pia wamempongeza Rais Samia kwa kutimiza miaka yake 66 ya kuzaliwa, huku wakimtakia afya njema, hekima na maisha marefu ili aendelee kuliongoza Taifa kwa busara na upendo.
Kwa upande wake Mratibu wa Taasisi ya Together for Samia, Nathaniel Maseke, amesema kuwa uwekezaji unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita unaonyesha dhamira ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwawezesha vijana kwa maarifa, ujuzi na fursa za kiuchumi huku akibainisha kuwa ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi katika maeneo mbalimbali nchini umeongeza nafasi kwa vijana kujifunza ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Maseke ameongeza kuwa Rais Dkt. Samia amefanya mabadiliko makubwa katika sekta muhimu ikiwemo afya, nishati, elimu na miundombinu, jambo lililochochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha huduma kwa wananchi huku akisisitiza kuwa kipaumbele cha Rais katika kuimarisha maridhiano, umoja na amani nchini kimeweka mazingira salama kwa vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo bila hofu.
Kwa upande wake, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana Innovation, Dorcas Richard, amesema kuwa Serikali imeendelea kufungua milango kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua inayoongeza ajira na fursa za biashara kwa vijana.
Amebainisha kuwa mikopo yenye riba ya asilimia mbili kwa vijana imekuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo, na kwamba vijana wengi tayari wananufaika na matunda ya sera hizo, huku akimpongeza Rais kwa kuendelea kufungua njia za mafanikio kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Nao, Vijana Ridhiwani Chakachaka na Hajrati Miraji, wakizungumza kwa niaba ya vijana wengine, wamesema kuwa juhudi za Rais Samia zimewezesha vijana kueleza malalamiko yao kwa njia ya amani na kupata suluhu bila migogoro.
"Kuanzishwa kwa Wizara ya Maendeleo ya Vijana kumeongeza sauti na nafasi ya vijana katika maamuzi ya Taifa, jambo lililotupa matumaini mapya ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo",Amesema Chakachaka.
Ameongeza kuwa vijana wanamuunga mkono Rais kwa asilimia 100 kwa kutambua mchango na umuhimu wao, na kwa kuwa kiongozi anayejali mustakabali wa kizazi kijacho.
Kwa upande wa wanawake,Hajira amesema kuwa uongozi wa Rais Samia umeleta hamasa kubwa kwa wanawake kushiriki katika uongozi na shughuli za kiuchumi, kijamii na kiafya.
"Wanawake sasa tunaona nafasi yetu katika ujenzi wa Taifa na tunajisikia kuthaminiwa, hali iliyoongeza ari ya kufanya kazi kwa bidii",Amesema.
Hafla hiyo ilienda sambamba na maombi ya kumuombea Rais Dk.Samia aendelee kuiongoza Tanzania kwa amani, huku wazee na vijana wakiahidi kushirikiana kudumisha upendo, mshikamano na amani kwa maendeleo ya Taifa.




Comments
Post a Comment