CHALAMILA ASIKILIZA NA KUTATATUA KERO ZA WANANCHI NYAKASANGWE AHAIDI KUZITATUA.

 


Na.Mwandishi wetu

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amefanya ziara ya kikazi katika kata kadhaa za Manispaa ya Kinondoni kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili, hususan migogoro ya ardhi na upatikanaji wa huduma za jamii.


Akizungumza na wananchi wa Nyakasangwe na maeneo ya jirani leo Januari 13,2026 Chalamila amesema ziara hizo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ya kusogeza huduma karibu na wananchi na kusikiliza kero zao moja kwa moja badala ya kutegemea taarifa za maandishi pekee.

Chalamila amesisitiza kuwa ofisi yake iko wazi kwa wananchi wote na kwamba hatahofia kuchukua hatua dhidi ya yeyote atakayebainika kuvunja sheria au kunyang’anya haki za wengine, akisema haki lazima itendeke bila kujali mtu ni nani au ana nafasi gani katika jamii.

Aidha Chalamila ametolea mfano mgogoro wa ardhi uliotokea eneo la Kunduchi, ambapo alilazimika kuingilia kati na kubaini kuwa nyumba iliyokuwa inagombaniwa ilikuwa mali halali ya watoto wa familia moja, hivyo kuamuru irejeshwe kwa wamiliki halali kwa mujibu wa sheria.


Mkuu huyo wa mkoa amesema migogoro mingi ya ardhi Dar es Salaam inachangiwa na tamaa, udanganyifu na matumizi ya watu wanaojifanya mawakili au madalali, wanaowapotosha wananchi kwa lengo la kujipatia fedha, jambo linalochelewesha haki kupatikana.



Chalamila amewaonya wananchi kuacha tabia ya kujiona wanyonge mbele ya sheria, akisema kila Mtanzania ana haki sawa bila kujali ana uwezo mkubwa wa kifedha au la, na kwamba vyombo vya dola vipo kwa ajili ya kuwatumikia wote kwa usawa.

Ametoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni kuandaa orodha ya migogoro mikubwa ya ardhi ili ichunguzwe na kutatuliwa kwa haraka, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kumiliki hati miliki za viwanja ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaletea wananchi miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, kituo cha afya na mahakama ya mwanzo katika maeneo ya Nyakasangwe na Madale.

Meya wa Manispaa ya Kinondoni alisema upimaji wa viwanja katika maeneo hayo ulifanyika tangu mwaka 2017 na kampuni binafsi, lakini changamoto iliyopo ni wananchi wengi bado hawajapata hati miliki, hali inayochochea migogoro ya muda mrefu.

Naye Diwani wa Kata ya Wazo, Grace Mkumbwa, aliomba wakandarasi kukamilisha miradi ya barabara kwa wakati na kuhakikisha taa za barabarani zinawekwa kwa ajili ya usalama, akisisitiza kuwa miundombinu bora na upatikanaji wa hati miliki ni msingi wa maendeleo ya wananchi.



Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.