MAKONDA: CAF KUFANYA MKUTANO TANZANIA, UWEKEZAJI WA SAMIA WAVUTIA AFRIKA.
Na. Sophia Kingimali.
Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Tanzania imeendelea kupata heshima kubwa kimataifa kufuatia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika sekta ya michezo hususan mpira wa miguu na kupelekea wajumbe wa kamati tendaji ya CAF kuja nchini kwa ajili ya mikutano yake.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Januari 9,2026 Makonda amesema kuwa Januari 16, Rais Samia alituma ujumbe maalum kwa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe, ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wake mkubwa katika kuendeleza soka barani Afrika na kuhamasisha amani kupitia michezo.
Amesema ujumbe huo uliainisha dhamira ya dhati ya Rais Samia kuendelea kuwekeza bila kujali gharama ili kuhakikisha Tanzania inakuwa miongoni mwa mataifa makubwa ya soka Afrika na hata duniani, jambo lililompa Motsepe msukumo wa kushirikiana kwa karibu na Tanzania.
Makonda ameeleza kuwa ushirikiano huo uliwezesha pande hizo kukutana na kujadiliana masuala mbalimbali ikiwemo ombi la CAF kufanya mikutano yake mikuu nchini Tanzania, hatua inayotokana na kuvutiwa na maendeleo makubwa ya miundombinu ya michezo.
Alifafanua kuwa kwa sasa Serikali inawekeza takribani shilingi trilioni 1.76 katika ujenzi na ukarabati wa viwanja vya michezo katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Dar es Salaam, sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya barabara na huduma zinazozunguka viwanja hivyo.
Makonda alisema tayari Rais wa CAF ameonesha nia ya kuja Tanzania kwa ajili ya mkutano wa Kamati Tendaji wa shirikisho hilo, ambapo timu za awali zinaanza kuwasili Dar es Salaam kuanzia tarehe 9, huku mkutano ukitarajiwa kufanyika Februari 13 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Ameongeza kuwa ujio wa viongozi hao ni fursa kubwa kwa Tanzania kujitangaza kama taifa salama, lenye amani na linalowekeza kwa vitendo katika michezo, pamoja na kutoa nafasi ya kupata msaada wa kitaalamu na kuhakikisha viwango vya CAF vinazingatiwa kikamilifu.
Makonda amesema maandalizi yote yanaendelea chini ya usimamizi wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ili kuhakikisha wageni hao wanapokelewa kwa heshima inayostahili kuanzia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere hadi maeneo watakayofikia.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambuliwa kimataifa, kupewa tuzo na kuendelea kujenga diplomasia ya michezo inayofanya sekta hiyo kuwa miongoni mwa sekta kumi bora zinazochangia maendeleo ya taifa.

Comments
Post a Comment