MKUU WA MKOA DSM AITA WAWEKEZAJI SEKTA YA AFYA.
Na.Mwandishi Wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametoa wito umetolewa kwa wawekezaji katika sekta ya afya kuja kuwekeza jijini Dar es Salaam (DSM) ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora za tiba, ajira na kuchochea uchumi wa mkoa huo.
Wito huoameutoa leo Januari 12,2026 Jijini Dar es salaam,wakati wa ziara yake katika Hospitali ya Shifaa, Chalamila amesema Mkoa una uhitaji mkubwa wa hospitali za kisasa kutokana na ongezeko la watu na mahitaji mapya ya huduma za afya, hivyo ni fursa adhimu kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Amesema mazingira ya uwekezaji katika mkoa huo yameboreshwa, huku serikali ikiendelea kuweka sera na kanuni rafiki zinazowezesha sekta binafsi kuwekeza kwa urahisi katika miradi ya afya ikiwemo hospitali, vituo vya afya na viwanda vya dawa.
Chalamila amewapongeza wawekezaji wa Hospitali ya Shifaa kwa uwekezaji wao wa zaidi ya dola za Marekani milioni 60, akisema hospitali hiyo ni mfano wa uwekezaji wenye tija unaosaidia kuboresha maisha ya wananchi na kupunguza gharama za kusafiri nje ya nchi kutafuta matibabu.
Ameeleza kuwa uwekezaji katika afya hauishii kwenye kutoa huduma pekee, bali pia huleta ajira kwa madaktari, wauguzi na wataalamu wengine, pamoja na kuchochea maendeleo ya rasilimali watu ambayo ni msingi wa uchumi wa taifa.
Mkuu huyo wa mkoa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi (PPP), akisema badala ya serikali kujenga hospitali mpya kila eneo, inaweza kushirikiana na wawekezaji waliopo ili kupanua huduma kwa gharama ndogo na ufanisi zaidi.
Ameongeza kuwa uwekezaji wa afya unahitaji nguzo tatu muhimu ambazo ni rasilimali watu, miundombinu na vifaa tiba vya kisasa, huku serikali ikiahidi kuendelea kuweka mazingira wezeshi ili wawekezaji waweze kupata vibali na huduma kwa wakati.
Aidha amewahamasisha wananchi kuwa na bima ya afya ili kuongeza uwezo wa kupata matibabu katika hospitali binafsi na za serikali, akisema mpango wa bima ni sehemu ya mkakati wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania wengi zaidi.
Amehitimisha kwa kutoa wito kwa wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza katika sekta ya afya kufika Dar es Salaam, akisisitiza kuwa mkoa uko tayari kushirikiana nao kwa karibu ili kuhakikisha miradi yao inafanikiwa na kunufaisha taifa kwa ujumla.

Comments
Post a Comment