WADAU WATAKIWA KUCHUKUA HATUA KUELEKEA MVUA ZA MASIKA .
Na.Mwandishi Wetu.
Tahadhari imetolewa kwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali kujiandaa kikamilifu kuelekea msimu mpya wa mvua za Masika, kutokana na uwezekano wa kutokea matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa na mafuriko.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 5,2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Ladislaus Chang’ wakati akitoa mwelekeo wa mvua za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei.amesema tathmini ya mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kwa msimu wa Masika mwaka huu, maeneo mengi nchini yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu kidogo ya wastani, huku baadhi ya maeneo yakitarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani.
"Pamoja na makadirio hayo, bado kuna uwezekano wa kutokea vipindi vifupi vya mvua kubwa katika maeneo mbalimbali nchini",Amesema.
Amesema kwa upande wa ukanda wa Ziwa Victoria unaojumuisha mikoa ya Kagera na Geita, Dk. Chang’a alisema maeneo hayo yanatarajiwa kupata mvua za wastani, huku mikoa ya Shinyanga ikitarajiwa kupata mvua za wastani kwenda chini kidogo ya wastani. Aliongeza kuwa mvua katika ukanda huo zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya Machi na kuendelea hadi Mei.
Katika nyanda za juu kaskazini mashariki zinazojumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani kwenda chini kidogo ya wastani, huku zikianza kati ya wiki ya pili na ya tatu ya Machi na kuisha mwishoni mwa Mei. Aidha, ukanda wa pwani ya kaskazini unaojumuisha Tanga, Dar es Salaam, Pwani na kaskazini mwa Morogoro unatarajiwa kupata mvua kuanzia wiki ya pili ya Machi hadi wiki ya nne ya Mei na wiki ya kwanza ya Juni.
Dk. Chang’a alibainisha kuwa mabadiliko ya hali ya hewa yanaendelea kuongeza uwezekano wa matukio ya hali mbaya ya hewa, hivyo hata maeneo yanayotabiriwa kupata mvua za wastani yanaweza kukumbwa na mvua kubwa zisizotarajiwa. Alisema mwezi Aprili unatarajiwa kuwa na ongezeko kubwa la mvua katika maeneo mengi ya nchi.
Kwa sekta ya kilimo na usalama wa chakula, TMA imetoa ushauri kwa wakulima kuandaa mashamba mapema, kutumia mbinu bora za kilimo na kuchukua tahadhari za kuzuia mmomonyoko wa udongo pamoja na upotevu wa rutuba. Pia wakulima wametakiwa kufuatilia kwa karibu taarifa za utabiri wa hali ya hewa ili kupanga ratiba za upandaji na uvunaji.
Kwa upande wa mifugo, Dk. Chang’a ameonya kuhusu uwezekano wa kutokea upungufu wa maji na malisho katika maeneo yatakayopata mvua chini ya wastani, hali inayoweza kusababisha migogoro ya matumizi ya rasilimali. Pia alitahadharisha kuhusu uwezekano wa milipuko ya magonjwa ya mifugo na kuongezeka kwa wadudu waharibifu katika maeneo yatakayopata mvua nyingi.
Katika sekta za ujenzi, usafiri, afya na usimamizi wa maafa, TMA imesisitiza umuhimu wa kuzingatia taarifa za tahadhari na utabiri wa kila siku ili kupunguza athari za mafuriko, uharibifu wa miundombinu na hatari za kiafya. Dk. Chang’a aliwataka viongozi wa serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla kuimarisha maandalizi na ushirikiano, pamoja na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa wakati ili kuokoa mali na maisha.



Comments
Post a Comment