WANAFUNZI KUKAA CHINI SIO UHABA WA FEDHA,NI UKOSEFU WA MIPANGO:CHALAMILA.
Na.Mwandishi Wetu.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila,ameagiza halmashauri ya Kinondoni kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini kwa kukosa madawati, akisema tatizo hilo halitokani na uhaba wa fedha bali ni ukosefu wa mipango sahihi na matumizi duni ya makusanyo ya mapato ya ndani.
Akizungumza leo Januari 12,2026 wakati wa uzinduzi wa mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Tandale, Chalamila amewapongeza viongozi wa mkoa, wilaya, mbunge na diwani kwa ushirikiano mzuri uliosaidia kufanikisha mradi huo, akieleza kuwa maendeleo hayo yametokana na uchapakazi na maono ya pamoja ya serikali na viongozi wa eneo hilo.
Chalamila amesema ongezeko la idadi ya watu linahitaji mipango ya muda mrefu katika sekta ya elimu, akibainisha kuwa madarasa ya msingi yataungana na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza, hali itakayolazimu uwepo wa miundombinu ya kutosha ikiwemo madarasa na mabweni.
Chalamila pi,amehimiza ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa shule kupitia uwekezaji wa kijamii (Corporate Social Investment), akisisitiza kuwa makampuni yanapaswa kuwekeza katika elimu kama njia ya kuchangia maendeleo ya taifa.
Pia ameagiza kuwepo kwa mipango ya mazoezi na michezo kwa wanafunzi, akieleza kuwa shule nyingi za mijini hazina viwanja vya michezo jambo linaloweza kuathiri afya za wanafunzi licha ya kuwa na uwezo mzuri wa kitaaluma.
Chalamila alitoa maagizo ya kupanga mazingira ya miji kwa kudhibiti wafanyabiashara wanaozunguka maeneo ya shule, akisema mazingira yasiyo rasmi yanaweza kuathiri nidhamu na usalama wa wanafunzi.
Maagizo hayo yamelenga kuimarisha mipango ya elimu na maendeleo ya miundombinu katika Manispaa ya Kinondoni hususan eneo la Tandale, akisisitiza ujenzi wa maghorofa ya shule kama ajenda ya kudumu ili kukabiliana na ongezeko kubwa la idadi ya wanafunzi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni Hanifa Hamza amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa maelekezo hayo, akiahidi kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na wadau wote wa elimu ili kuhakikisha ongezeko la wanafunzi linaendana na upatikanaji wa huduma bora za elimu na mazingira salama ya kujifunzia.


Comments
Post a Comment