Chalamila Aanzisha Operesheni Maalum Kupambana na Utapeli wa Ardhi Dar es Salaam.
Na.SOPHIA KINGIMALI
Mkuu wa Mkoa Dar kuanza marathon ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kuanza rasmi kwa operesheni maalum ya kusikiliza na kutatua kero za ardhi na vitendo vya utapeli vinavyowaumiza wananchi wa mkoa huo, lengo likiwa ni kurejesha haki na kuondoa mtandao wa wanyang’anyi waliodumu kwa miaka mingi.
Akizungumza na waandishi wa habari, leo Machi 2,2026 Jijini Dar es salaam Chalamila amesema kumekuwepo na kiwango kikubwa cha utapeli na unyang’anyi wa ardhi unaofanywa na makundi yanayoshirikiana na baadhi ya watu ndani na nje ya mifumo ya kiutendaji.
"Tayari baadhi ya waliokuwa wamepora ardhi wameanza kujitokeza na kuzirudisha kwa hiari, ambapo hadi sasa viwanja visivyopungua 19 vimerudishwa kimya kimya kwa wahusika halali",Amesema Chalamila.
Aidha Chalamila amebainisha kuwa makundi yaliyoathirika zaidi ni wajane, yatima, walinzi na familia zisizojiweza, ambao mara nyingi hunyang’anywa mali kwa kutumia nyaraka za kughushi au mikataba ya hila. “Hatuwezi kuruhusu Dar es Salaam ijengwe juu ya msingi wa dhuluma na choyo,” amesisitiza.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa wiki moja kwa watu wanaojua wanamiliki ardhi isiyo yao kujitokeza na kuirejesha kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunguliwa mashtaka ya jinai na utakatishaji wa fedha kwani amesema orodha ya wahusika tayari ipo na uchunguzi wa kina umekamilika.
Mbali na ardhi, Chalamila amegusia utapeli katika biashara ya magari, akieleza kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakilipa mamilioni ya shilingi kwa magari yanayodaiwa kuwa bandarini, lakini baadaye kubainika kuwa hayapo au hayajalipiwa ushuru amelitoa mfano wa mwananchi aliyedhulumiwa zaidi ya Sh milioni 100 katika mazingira hayo.
Amesema pia kumebainika kuwepo kwa mikopo kandamizi inayowalazimisha wakopaji kusaini mikataba miwili kwa wakati mmoja—wa mkopo na wa mauziano ya dhamana—hali inayosababisha kupoteza mali zao kwa muda mfupi hivyo ameahidi kushirikiana na vyombo husika kudhibiti tabia hiyo.
Chalamila ametangaza kuwa kuanzia Machi 2 atakuwa akipokea malalamiko binafsi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, akiwataka wananchi kuwasilisha nyaraka zote kabla ya kuanza ziara ya “mguu kwa mguu” itakayoanza Machi 9 kukagua maeneo yenye migogoro katika wilaya za Kinondoni, Ilala na Temeke.
Aidha ameshukuru ushirikiano anaoupata kutoka Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, TAKUKURU na vyombo vya ulinzi na usalama, akisema mapambano hayo yanahitaji nguvu ya pamoja ili kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake bila kumuonea mtu.
Katika kuonesha dhamira ya Serikali, Chalamila alisema Rais Samia Suluhu Hassan amesisitiza viongozi kusimamia haki na kulinda rasilimali za wananchi, na kwamba operesheni hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo hilo katika ngazi ya mkoa.
Sambamba na hayo Chalamila ametoa wito kwa wananchi wa Dar es Salaam na hata kutoka mikoa mingine wenye migogoro inayohusiana na ardhi ndani ya jiji hilo kufika ofisini kwake ili kusaidiwa, akiahidi kuwa hakuna aliye juu ya sheria na haki itatendeka bila upendeleo.



Comments
Post a Comment