DCEA yakamata tani 9.93 za dawa za lulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya.

 



Na.Sophia Kingimali.


Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini imetangaza kukamata tani 9.93 za dawa za kulevya aina mbalimbali pamoja na chupa 1,795 za dawa tiba zenye asili ya kulevya katika kipindi cha Januari na Februari 2026. 

Operesheni hizo pia zimefanikisha kuteketezwa kwa ekari 87.5 za mashamba ya bangi, kukamatwa kwa magari sita na pikipiki 29 zilizotumika katika usafirishaji wa dawa hizo, huku jumla ya watuhumiwa 151 wakitiwa mbaroni katika mikoa mbalimbali nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mach 4,2026 Jijini Dar es salaam Kamishna Jenerali Aretas Lyimo amesema mafanikio hayo yanatokana na operesheni maalum zilizofanyika kwa ushirikiano wa vyombo vya ulinzi na usalama. 

Amesema Katika operesheni ya pamoja na maafisa wa forodha wa kituo cha Mutukula, zilikamatwa boksi 105 za dawa aina ya Pethidine zenye chupa 1,045, boksi 31 za Morphine Sulphate zenye chupa 310 na boksi 44 za Fentanyl zenye chupa 440. Dawa hizo zilikutwa ndani ya basi la abiria la kampuni ya SR Classic lenye usajili wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lililokuwa likiingia nchini kutoka Uganda.

"Watuhumiwa saba walikamatwa kuhusiana na tukio hilo, akiwemo Hassan Omary Mwambashi maarufu Macheni (50) mkazi wa Mbezi, pamoja na wenzake kutoka Dar es Salaam, Tanga na Uganda. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kinyume cha sheria na taratibu za nchi",Amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Mamlaka imefafanua kuwa dawa aina ya Pethidine, Morphine na Fentanyl ni dawa zenye asili ya afyuni (opioids) zinazotumika hospitalini kwa ajili ya kupunguza maumivu makali kwa wagonjwa wa saratani, ajali na selimundu. Hata hivyo, dawa hizo zinapochepushwa zinaweza kusababisha utegemezi mkubwa na madhara makubwa kiafya kutokana na nguvu yake.

Katika kukabiliana na bangi aina ya skanka, operesheni zilizofanyika jijini Dar es Salaam zilimkamata mtuhumiwa mmoja akiwa na kilo zaidi ya 81 za dawa hiyo zilizokuwa zimefichwa ndani ya lori lililobeba matunda. 

Aidha, katika maeneo ya Chanika Buyuni na jijini Mbeya, watuhumiwa kadhaa walikamatwa wakisafirisha jumla ya mamia ya kilo za skanka kupitia mabasi ya abiria.

Operesheni hizo pia zilifanyika katika mikoa ya Arusha, Tabora, Mwanza, Tanga na mingine ambako zilikamatwa tani kadhaa za bangi na mirungi pamoja na kiasi kidogo cha heroin. Mamlaka imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana na taasisi za Serikali na jamii kwa ujumla kuhakikisha dawa za kulevya na dawa tiba zenye asili ya kulevya hazichepushwi, huku ikiitaka jamii kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya biashara hiyo haramu.

Aidha Mamlaka hiyo  itaendelea kuimarisha doria na ukaguzi katika mipaka na barabara kuu ili kudhibiti mtandao wa usafirishaji wa dawa za kulevya unaovuka mipaka ya nchi.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.