Wanawake TANESCO waaswa kuwa mabolozi wazuri wa nishati safi ya kupikia.
Na.Sophia Kingimali.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dorothy Gwajima, ametoa wito kwa wanawake watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuwa vinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akisisitiza kuwa wao ndio mabalozi muhimu wa mabadiliko kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Akizungumza leo March 4,2026 jijini Dar es salaam katika kongamano la wanawake wa TANESCO, Waziri Gwajima amesema shirika hilo lina mchango mkubwa katika maendeleo endelevu ya taifa na ustawi wa wanawake, hasa kupitia upatikanaji wa umeme unaorahisisha maisha na kuinua uchumi wa familia.
Ameipongeza kamati ya maandalizi kwa kufanikisha kongamano hilo na kueleza kuwa limekuja wakati muafaka kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake.
Waziri gwajima ameitaja ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ya kitaifa na haiwezi kufanikiwa bila ushiriki wa sekta zote, akiwemo wanawake wa TANESCO huku akisisitiza kuwa bila umeme wa uhakika katika kaya nyingi, mwanamke ataendelea kubeba mzigo wa kutumia kuni na mkaa, hali inayohatarisha afya na kupoteza muda wa kushiriki shughuli za maendeleo.
Aidha Gwajima ameeleza kuwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 zinaonesha asilimia 81 ya kaya nchini bado zinatumia kuni na mkaa kupikia, ambapo asilimia 55 hutumia kuni na asilimia 26 mkaa amesema hali hiyo ni changamoto kubwa inayohitaji mapinduzi ya haraka ya fikra na utekelezaji wa mikakati madhubuti.
Amebainisha kuwa matumizi ya umeme kwa kupikia bado ni madogo, yakifikia takribani asilimia 4.3 tu, huku gesi ikitumiwa na asilimia 9.4 ya kaya. Hivyo, ametoa wito kwa TANESCO kushirikiana na wizara yake na wadau wengine kuhakikisha takwimu hizo zinabadilika kabla ya mwaka 2034.
Waziri Gwajima alikumbusha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, tayari alizindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo la kufikisha asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ifikapo mwaka 2034.
Amesema utekelezaji wa mkakati huo unahitaji mshikamano wa kweli, hasa kutoka kwa taasisi kama TANESCO.
Aliwataka wanawake wa TANESCO kuanza mabadiliko hayo majumbani kwao ili wawe mfano kwa jamii.
“Anzeni nyumbani, muwe mabalozi wa nishati safi. Jamii ikiona nyinyi mnatumia majiko ya umeme kwa mafanikio, wataamini na kufuata,” amesisitiza waziri Gwajima.
Aidha, ameeleza kuwa zipo dhana potofu kuwa kupikia kwa umeme ni gharama kubwa, akisema teknolojia ya sasa imeleta majiko yanayotumia umeme kidogo na kwa gharama nafuu hivyo ametoa rai kwa TANESCO kuongeza kampeni za uelimishaji ili kuondoa hofu hiyo kwa wananchi.
Kwa upande wa uwezeshaji, Waziri huyo ametaja programu za TANESCO zinazowezesha wateja kukopeshwa majiko ya umeme na kulipia kidogo kidogo kupitia ununuzi wa umeme au makato ya mishahara kwa watumishi.
Amesema programu hizo zitasaidia wanawake wa kipato cha chini kuanza kutumia nishati safi bila mzigo mkubwa wa kifedha.
Aidha Gwajima amesisitiza kuwa nishati safi si suala la mazingira pekee, bali ni ajenda ya afya, uchumi na usawa wa kijinsia,ameeleza kuwa mwanamke anapotumia nishati safi huokoa muda, hulinda afya yake na hupata nafasi zaidi ya kushiriki shughuli za uzalishaji na malezi bora ya familia.
Ameongeza kuwa wizara yake itashirikiana na maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata na vijiji kupeleka elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya umeme kupikia Lengo likiwa ni kubadili mitazamo hasi na kuhamasisha jamii kukumbatia mabadiliko hayo.
Waziri Gwajima pia amewataka wanawake wa TANESCO kuendelea kuwa chachu ya mageuzi katika sekta ya nishati, akisisitiza kuwa mafanikio ya ajenda ya nishati safi yatategemea juhudi zao kama mabalozi wa mabadiliko.
“Maendeleo ya taifa hayawezi kuwa jumuishi bila mwanamke kushiriki kikamilifu, na nishati safi ni sehemu ya ukombozi wake,” amehitimisha waziri Gwajima.





Comments
Post a Comment