BoT Yabaki na Riba ya Asilimia 5.75 Kukabili Changamoto za Uchumi wa Dunia.

 


Na Sophia Kingimali.


Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania(BoT) imeendelea kuonesha msimamo wa tahadhari katika usimamizi wa uchumi baada ya kuamua kubakiza kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) katika asilimia 5.75 kwa robo ya pili ya mwaka 2026.

Uamuzi huo unaakisi jitihada za mamlaka ya fedha kulinda uthabiti wa uchumi huku kukiwa na changamoto zinazoendelea katika mazingira ya uchumi wa dunia, hususan migogoro ya kisiasa inayoathiri biashara na uwekezaji.

Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ilifikia uamuzi huo baada ya kufanya tathmini ya kina ya mwenendo wa uchumi wa ndani na nje, ikibaini kuwa kiwango hicho bado kinafaa katika kipindi cha sasa.

Akizungumza leo Aprili 2, 2026, Naibu Gavana wa Benki Kuu anayesimamia Sera za Fedha na Uchumi, Dkt. Yamungu Kayandabila, amesema lengo kuu ni kuhakikisha mfumuko wa bei unaendelea kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3 hadi 5.

Ameeleza kuwa uthabiti wa riba hiyo pia utasaidia kupunguza madhara yanayotokana na misukosuko ya kiuchumi duniani, ikiwemo athari za mgogoro unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati.

Aidha Dkt. Kayandabila amesema, migogoro hiyo imeanza kuathiri baadhi ya sekta muhimu kama biashara na uwekezaji, hali inayoweza kuwa na madhara ya moja kwa moja kwa uchumi wa Tanzania endapo haitadhibitiwa.

Amesema Pamoja na changamoto hizo, uchumi wa Tanzania umeendelea kuonesha kuimarika, ambapo ukuaji wa Pato la Taifa unakadiriwa kufikia asilimia 6.2 kwa Tanzania Bara na asilimia 6.7 kwa Zanzibar katika robo ya kwanza ya mwaka 2026.

"Ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na sekta za ujenzi, kilimo, huduma za fedha na bima pamoja na utalii, huku wadau wa sekta ya benki wakipongeza juhudi za Benki Kuu katika kudumisha utulivu wa mfumo wa fedha nchini".Amesema

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.