Mitandao mipya ya dawa za kulevya yaibuliwa; DCEA yaonya matumizi ya mbinu za kisasa usafirishaji

 


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam


MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imebaini kuibuka kwa mitandao mipya ya usafirishaji wa dawa za kulevya inayotumia mbinu za kisasa kuficha bidhaa hizo haramu, hali inayozua tahadhari mpya kwa vyombo vya usalama na wananchi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema wahalifu wameanza kutumia njia zisizo za kawaida kusafirisha dawa hizo, ikiwemo kuzificha kwenye mizigo ya nguo za mitumba, matunda kama maembe, pamoja na ndani ya mifumo ya hewa (AC) ya mabasi.

Amesema mabadiliko hayo ya mbinu yanakuja kufuatia kuimarishwa kwa udhibiti katika bandari na mipaka, jambo lililowalazimu wahusika wa biashara hiyo kubuni njia mbadala za kusafirisha dawa hizo ndani ya nchi.

“Tunashuhudia wahalifu wakibadilika na kuja na mbinu mpya kila wakati, lakini sisi pia tunaendelea kuimarisha mikakati ya kukabiliana nao,” amesema Lyimo.

Katika operesheni zilizofanyika mwezi Machi 2026, mamlaka hiyo ilifanikiwa kukamata kilogramu 1,983.31 za dawa za kulevya pamoja na kemikali bashirifu zinazoweza kutumika kuzalisha dawa hizo, hatua inayotafsiriwa kama juhudi za kukabiliana na mtandao huo mpya.

Amesema aina ya dawa iliyoongezeka zaidi ni mirungi iliyofikia kilogramu 1,267.12, sawa na asilimia 64 ya dawa zote zilizokamatwa, ikionesha mwelekeo mpya wa soko la dawa hizo.

Mbali na hilo, mamlaka ilikamata pia vidonge 286 na chupa 1,001 za dawa tiba zenye asili ya kulevya, zikiwemo benzodiazepine na opioid kama tramadol na codeine, ambazo hutumiwa vibaya na kusababisha uraibu.

Operesheni hizo zilifanyika katika mikoa mbalimbali ikiwemo Pwani, Mwanza, Dar es Salaam, Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Songwe, huku baadhi ya dawa hizo zikielekezwa katika soko la Dar es Salaam.

Sambamba na hayo, ekari 55.5 za mashamba ya bangi ziliteketezwa na watuhumiwa 77 kukamatwa, sambamba na vyombo vya usafiri vilivyotumika katika mtandao huo kukamatwa.

Kutokana na hali hiyo, Lyimo amesisitiza kuwa mamlaka itaendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kuvunja mitandao hiyo na kuwachukulia hatua kali wahusika wote bila kujali hadhi zao.

Vilevile, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na mamlaka kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufichua mitandao hiyo, akibainisha kuwa ushirikiano wa jamii ni silaha muhimu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.