POSTA NA BODI YA MIKOPO ZASAINI USHIRIKIANO KURAHISISHA HUDUMA KWA VIJANA
Na Sophia Kingimali
Dar es Salaam.
Taasisi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu(HESLB) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Posta Tanzania, hatua inayolenga kurahisisha huduma za maombi ya mikopo kwa vijana nchini.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo,leo Aprili 22,2026 Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo,(HESLB) Dk. Bill Kiwia, amesema, ushirikiano huo na Posta utasaidia kutoa suluhisho kwa changamoto mbalimbali walizokuwa wakipata wanafunzi pindi wanapoomba mikopo hiyo.
Amesema ofisi hizo zitatumika kusaidia vijana kujaza na kuwasilisha maombi ya mikopo, kufanya uhakiki wa nyaraka na kutoa msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha wanakidhi vigezo vinavyohitajika.
“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna kijana anayekosa mkopo kwa sababu ya changamoto za kiufundi au kukosa msaada wa kujaza maombi,” alisisitiza Dk. Kiwia.
Amesema tangu kuanzishwa kwa bodi hiyo, zaidi ya trilioni tisa zimetolewa kama mikopo kwa wanufaika zaidi ya milioni moja, wakiwemo wanafunzi wa shahada, stashahada, uzamili na uzamivu.
Aidha, ameeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kumekuwepo na changamoto katika mifumo ya maombi, hasa kwa vijana walioko maeneo ya vijijini na wasio na urahisi wa kupata huduma za mtandao.
Kwa upande wake, Postamasta Mkuu Macrice Mbodo amesema shirika hilo linaendelea kutekeleza wajibu wake wa kurahisisha huduma kwa wananchi kupitia mtandao wake wenye zaidi ya ofisi 350 nchini na kuunganishwa na mtandao wa kimataifa.
Alibainisha kuwa Posta tayari inashirikiana na taasisi zaidi ya 150, zikiwemo za serikali na binafsi, kusambaza huduma mbalimbali kama vile vifaa tiba, taarifa na huduma za kifedha.
Alisema kupitia ushirikiano huo mpya, watahakikisha vijana wanapata mwongozo sahihi wa kujaza fomu za mikopo na kuepuka makosa yanayoweza kuwanyima fursa hiyo muhimu.
Hafla hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kukuza maendeleo ya vijana nchini.





Comments
Post a Comment