VIONGOZI WA SERIKALI NA KIROHO WANG’ARA MAADHIMISHO YA MIAKA 19 YA WRM JIJINI DAR ES SALAAM
Na.Mwandishi wetu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu ameongoza viongozi mbalimbali wa serikali na kisiasa kushiriki maadhimisho ya miaka 19 ya Kanisa la WRC yanayoendelea katika kanisa hilo kivule Jijini Dar es salaam.
Katika tukio hilo, Sangu aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, Mbunge wa Kivule, Ojambi Massaburi pamoja na Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, ambapo walipokelewa na waumini na viongozi wa kanisa hilo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mpogolo alisema kutimiza miaka 19 kwa Kanisa la WRC ni historia kubwa inayostahili pongezi, akiwashukuru pia viongozi wa kanisa hilo kwa mchango wao mkubwa katika kuimarisha huduma za kiroho na maendeleo ya kijamii katika mkoa huo.
Ameongeza kuwa uwepo wa viongozi hao umekuwa chachu ya amani na maendeleo nchini, huku akibainisha kuwa serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za kidini katika kujenga jamii yenye mshikamano.
Aidha, amegusia changamoto za baadhi ya matukio ya uhalifu yanayosambaa kwa kasi mitandaoni, akisisitiza kuwa mamlaka za wilaya zitachukua hatua kwa kufanya uchunguzi pamoja na kutoa msaada kwa waathirika.
Mpogolo amewataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa na kukemea vitendo viovu, akieleza kuwa maombi yana nafasi kubwa katika kuimarisha maadili ya jamii na kuondoa changamoto zinazoikabili.
Kwa upande wake, Ester Bulaya amesema maadhimisho hayo ni tafsiri halisi ya kumtumikia Mungu, akiahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za viongozi wa dini huku akieleza kuwa hata Rais anaunga mkono mchango wao kutokana na nafasi yao katika kuliombea taifa.
Naye Mbunge wa kivule Ojambi Massaburi ameeleza kuwa ni miongoni mwa wale waliokuzwa kiimani na Askofu Nicklous Suguye, akisisitiza kuwa maombi na malezi ya kiroho aliyoyapata yamechangia mafanikio yake katika nafasi mbalimbali za uongozi alizowahi kushika.



Comments
Post a Comment