Msajili wa Hazina, Fitch Ratings watathmini mageuzi ya taasisi za umma
Na Mwandishi wa OTR Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) Jumanne, Agosti 11, 2026, ilifanya mazungumzo na kampuni ya Fitch Ratings Ltd ikiwa ni sehemu ya mapitio ya pili ya mwaka 2026 ya tathmini ya Fitch Ratings, katika mchakato unaohusisha taasisi mbalimbali za Serikali. Mazungumzo hayo yanalenga kuwapa wachambuzi wa Fitch Ratings fursa ya kupata taarifa za kina kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania, utekelezaji wa sera za kibajeti na fedha, pamoja na mikakati ya Serikali katika usimamizi wa deni la Taifa. Kwa upande wa OTR, mjadala ulijikita katika utendaji wa taasisi za umma, mageuzi yanayoendelea, vihatarishi vya kifedha, pamoja na mtiririko wa fedha kati ya Serikali na taasisi za Umma. Mapema mwaka huu, Fitch Ratings iliendelea kuipa Tanzania daraja ‘B+’ kwa hadhi ya ulipaji wa madeni ya muda mrefu ya fedha za kigeni, ikitaja mwelekeo imara wa ukuaji wa uchumi na uwezo wa Serikali kukabiliana na changamoto za kifedha baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 20...