DCEA Yafichua Mtandao wa Uingizaji Kemikali Hatari nchini

 


Na Sophia Kingimali.


MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeeleza kuwa operesheni maalum iliyofanyika mwezi Aprili mwaka huu imefanikiwa kufichua mtandao wa uingizaji na usafirishaji wa kemikali bashirifu zilizokuwa zikielekezwa katika matumizi haramu ya utengenezaji wa dawa za kulevya nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Mei 13, 2026 jijini Dar es Salaam, Kamishina Jenerali wa DCEA, Aretas James Lyimo alisema mamlaka hiyo ilikamata lita 66,048 za kemikali mbalimbali zikiwemo Cyclohexanone na Extra Neutral Alcohol (ENA), ambazo licha ya kuwa na matumizi halali viwandani, zimekuwa zikitumiwa pia katika maabara haramu za kutengeneza dawa za kulevya.

Amesema operesheni hiyo ilitekelezwa kwa ushirikiano na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na TRA, ambapo magari mawili yaliyokuwa yakisafirisha kemikali hizo yalikamatwa sambamba na watuhumiwa wawili wanaohojiwa kuhusiana na tukio hilo.

Kwa mujibu wa DCEA, uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa baadhi ya kemikali hizo ziliingizwa nchini bila kufuata taratibu za kisheria, ikiwemo kutokuwa na vibali kutoka mamlaka husika, huku nyingine zikisafirishwa kwa kutumia vibali vya kughushi ili kuficha uhalisia wa mzigo uliokuwa ukisafirishwa.

Kamishina Lyimo alisema mbinu hizo zinaonyesha kuwepo kwa mitandao ya kihalifu inayotumia mianya mbalimbali kuingiza kemikali bashirifu kwa ajili ya kuzalisha dawa za kulevya, hali inayohatarisha usalama na afya ya jamii.

Amefafanua kuwa kemikali aina ya Cyclohexanone zina uwezo wa kutumika kuzalisha dawa za kulevya aina ya PCP, na kwamba kiasi kilichokamatwa kingeweza kutengeneza zaidi ya tani 11 za dawa hizo haramu.

Katika oparesheni nyingine zilizofanyika kwenye mikoa mbalimbali nchini, DCEA ilisema imekamata tani kadhaa za bangi na mirungi pamoja na kiasi cha heroin na cocaine, huku mashamba ya bangi yakiteketezwa na watuhumiwa zaidi ya 80 kutiwa mbaroni.

Mamlaka hiyo imeeleza kuwa itaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za Serikali katika kudhibiti uchepushaji wa kemikali bashirifu na biashara ya dawa za kulevya, huku wananchi wakitakiwa kuendelea kutoa taarifa zitakazosaidia kuvunja mitandao hiyo ya kihalifu.

Comments

Popular posts from this blog

HAPI AWATAKA WAGOMBEA WALIOKOSA UTEUZI KUVUNJA MAKUNDI NA KUUNGANA KUTAFUTA KURA ZA KISHINDO ZA CHAMA HICHO.

Msajili Hazina aipa tano TPA

YUSUPH RAI AWASII WANANCHI TEMEKE KUCHAGUA MTU SIO CHAMA KWA MAENDELEO YA JIMBO HILO.