BoT Yazindua Mfumo wa Kidijitali Kuimarisha Uwazi wa Biashara ya Fedha za Kigeni
Na.Mwandishi wetu
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua hatua mpya ya kuimarisha uwazi na ufanisi katika soko la fedha za kigeni baada ya kuzindua Mfumo wa Kielektroniki wa Kuoanisha Miamala (EMS), utakaorahisisha biashara ya fedha za kigeni kwa njia ya kidijitali.
Mfumo huo uliozinduliwa Juni 8, 2026, unatarajiwa kuongeza uwazi katika upangaji wa viwango vya ubadilishaji fedha huku ukiimarisha uwezo wa Benki Kuu kufuatilia mwenendo wa soko kwa wakati halisi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Gavana wa BoT anayesimamia Sera za Uchumi na Fedha, Dkt. Yamungu Kayanda Bila, alisema mfumo huo utawezesha washiriki wa soko kuwasilisha na kuoanisha miamala ya fedha za kigeni kwa njia ya kielektroniki, hatua itakayosaidia kuondoa changamoto za mfumo wa kawaida wa biashara.
Alisema EMS itachangia kuimarisha utulivu wa soko la fedha za kigeni kwa kuweka mazingira yenye ushindani wa haki na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa viwango vya ubadilishaji fedha.
Kwa mujibu wa BoT, washiriki wa mfumo huo ni mabenki ya biashara pamoja na wauzaji wakubwa wa bidhaa nje ya nchi watakaoidhinishwa kushiriki katika soko hilo.
Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa BoT, Emmanuel Akaro, alisema mfumo huo utatumia utaratibu wa biashara usiotambulisha wahusika moja kwa moja (anonymous trading), ambapo oda za ununuzi na uuzaji zitaoanishwa kwa kuzingatia bei na muda wa kuwasilishwa.
Alieleza kuwa hatua hiyo itaongeza uadilifu wa soko na kuondoa uwezekano wa upendeleo katika utekelezaji wa miamala ya fedha za kigeni.
Mfumo huo utatumika katika miamala ya papo kwa papo kati ya Shilingi ya Tanzania na Dola ya Marekani, ukiwa sehemu ya mageuzi yanayoendelea kufanywa na Benki Kuu katika sekta ya fedha.
Uzinduzi wa EMS unaongeza mafanikio mengine yaliyofikiwa katika soko la fedha za kigeni nchini, yakiwemo utekelezaji wa Sera ya Ushiriki wa Benki Kuu katika Soko la Jumla la Fedha za Kigeni ya mwaka 2023 pamoja na Kanuni za Maadili za mwaka 2024 zinazolenga kuzingatia viwango bora vya kimataifa.
Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa hatua hiyo inaweza kuongeza imani ya wawekezaji na wafanyabiashara katika mfumo wa fedha wa Tanzania kwa kuweka mazingira yenye uwazi zaidi katika biashara ya fedha za kigeni.



Comments
Post a Comment